By Israel Saria on May 11, 2014
Hatimaye Manchester City
wamefanikiwa kunyakua ubingwa wa England katika siku ya mwisho ya Ligi
Kuu, ambapo walikuwa wakihitaji pointi moja tu kutawazwa wafalme.
Vijana hao wa Manuel Pellegrini hawakufanya makosa walipoingia
uwanjani nyumbani dhidi ya West Ham, kwani Samin Nasri na nahodha
Vincent Kompany walihakikisha wanaipatia timu yao mabao, huku ngome
ikihakikisha haivuji.
Wakati City wakipata ushindi huo, Liverpool waliokuwa wakiunyemelea
ubingwa pia kwa kusubiri kuteleza kwa City, walianza vibaya baada ya
Martin Skirttel kujifunga bao walipocheza dhidi ya Newcastle United na
kuwafisha moyo washabiki dimbani Anfield.
Hata hivyo, Liverpool walizinduka baadaye, wakasawazisha kisha
kufunga bao la ushindi lakini kwa kuzingatia matokeo ya City, Liver
walishindwa kutimiza ndoto ya kutwaa ubingwa huo ambao waliupoteza tangu
1990.
City walikuwa wakipewa nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa huo, hasa
baada ya Liverpool kuteleza hivi karibuni kwa kukubali kichapo kutoka
kwa Chelsea, kabla ya mechi iliyopita kwenda sare ya 3-3 na Crystal
Palace katika mchezo ambao vijana wa Brendan Rodgers walikuwa wanaongoza
kwa mabao matatu kwa bila.
Nafasi ya tatu imekwenda kwa Chelsea ambao walianza vibaya mechi yao
ya mwisho dhidi ya Cardiff kwa kutangulia kufungwa, lakini walisawazisha
na kuongeza bao la ushindi katika kulindwa heshima yao. Nafasi ya nne
imeshikwa na Arsenal waliowalaza Norwich 2-0.
Timu hizo nne ndizo zimeingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL)
wakati Everton waliowafunga Hull mabao 2-0 na Tottenham Hotspur
waliowakandika Aston Villa 3-0 wamefuzu kucheza Ligi ya Europa.
Manchester United wamemaliza msimu kwa sare ya 1-1 na Southampton.
Swansea waliwakung’uta Sunderland 3-1, West Bromwich Albion wakalala 2-1
kwa Stoke na Fulham wakatoka 2-2 na Crystal Palace.Norwich wameungana
na Cardiff na Fulham kushuka daraja.
No comments:
Post a Comment