Tuesday, January 29, 2013

WAZIRI MKUU WA SOMALIA ANUSURIKA KATIKA SHAMBULIO LA BOMU


 

SOMALIA,
Mtu mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga nchini Somalia ambapo mshambuliaji amejilipua karibu na ofisi za waziri mkuu
Mlinzi mmoja aliyeshuhudia shambulio hilo alisema kuwa polisi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa.

Lakini kwa mujibu wa maafisa wa utawala, watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea karibu na makao ya Rais mjni Mogadishu.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Sheikh mjini Nairobi anasema kuwa maafisa wakuu wanaelezea kuwa lengo la mshambuliaji lilikuwa kulipua ofisi ya waziri mkuu Abdi Farah Shirdon.
Lakini wanajeshi waliokuwa wanashika doria walisema walimzuia kufika katika ofisi hiyo.
Aidha maafisa walidokeza kwamba mshambuliaji alijilipua alipokuwa anahojiwa katika kizuizi kimoja cha polisi karibu na ofisi hiyo.
Mshambuliaji alijilipua karibu na ukuta unaotenganisha ubalozi wa Ethiopia na makao ya waziri mkuu.

Majengo hayo mawili yako ndani ya eneo ambalo pia linahifadhi makaazi ya rais.
Idadi ya washambuliaji wa kujitoa mhanga imekuwa ikipungua tangu wanamgambo wa Al Shabaab kuondoka Mogadishu kuanzia Agosti 2011 lakini hili li dhihirsiho la changamoto inayowakabili maafisa wa usalama katika kupambana na wanamgambo hao.(BBC)

SUMAYE KUNYANG'ANYWA SHAMBA

 


PWANI-TANZANIA,
SHAMBA la Frederick Sumaye lililoko Kisarawe mkoani Pwani, liko hatarini kuchukuliwa na halmashauri ya wilaya hiyo na kuligawa upya, kutokana na Waziri Mkuu huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza.

Habari zilizothibitishwa na viongozi kadhaa wa Wilaya ya Kisarawe, zimeeleza kuwa shamba la Sumaye lililoko eneo la Vikurunge Kata ya Kiluvya, ni miongoni mwa mashamba yaliyoko kwenye orodha ya kunyang’anywa na kugawiwa upya.

Hata hivyo mwenyewe amesema kuwa hana taarifa ya mpango huo wa halmashauri kuwanyang’anya watu mashamba.

“Sijui chochote na nipo kanisani, Sijui hata hiyo notisi ya halmashauri kutaka kunyang’anya mashamba,” alisema na kukata simu.

Chanzo cha habari kilisema “Huu ni mpango wa halmashauri na tayari imeshatoa tangazo tangu mwaka jana. Ilitoa siku 60 tangu Desemba 30 mwaka jana kwa wamiliki wake kuyaendeleza mashamba hayo, baada ya hapo yatanyang’anywa,” chanzo cha habari kilieleza na kuendelea;

“Mheshimiwa Sumaye ni miongoni mwa wamiliki hao, yeye shamba lake lina zaidi ya ekari 40 na lipo eneo la Vikurunge Kata ya Kuluvya. Ameshindwa kuliendeleza kwa kipindi cha miaka mitano sasa.”

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makurunge, Jocline Mfuru alikiri Sumaye kumiliki eneo kubwa eneo hilo, lakini alisema taarifa zaidi zipo halmashauri ndio ambao wanajua zaidi kwani hata yeye mwenyewe ni mgeni katika nafasi hiyo ana mwezi mmoja tu tangu awepo hapo baada ya mtendaji wa awali kuondolewa.

“Sina muda mrefu katika nafasi yangu na ninatambua notisi ya siku 60 ya wale ambao hawajaendeleza mashamba lakini siwezi kuzungumzia zaidi kwani sina taarifa za kutosha,” alisema Mfuru.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe, Yona Maki alithibitisha kutekelezwa kwa operesheni hiyo na kusema kuwa sasa wapo katika hatua ya kufanya tathamini.
Akiwa amekwepa kuthibitisha kama shamba la Sumaye nalo litanyang’anywa, Maki alisema, “Ni kweli Sumaye anamiliki eneo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na amejenga nyumba ya kuishi.”

Aliendelea “Lakini, kujenga nyumba hakutoshi kueleza kuwa shamba hilo limeendelezwa. Tunapitia nyaraka zinazohusu umiliki wake na kuona kama lipo kwenye mpango huo au la.”
Maki alisema uchunguzi unaofanyika dhidi ya Sumaye ni pamoja na kujua aliomba kumilikisha eneo hilo kwa ajili ya shughuli gani na kuangalia iwapo kile alichoombea ndicho anachokitekeleza.

“Nipe muda niweze kujua alimilikishwa kwa ajili ya utekelezaji wa jambo gani na kama hicho alichoombea ndicho anachokifanya,” alisema Maki.

Maki alifafanua kuwa hatua ya kupitia upya umiliki wa mashamba wilayani humo na uendelezwaji wake, inafanyika kwa mujibu wa sheria ya vijiji na miji namba 4 na 5 ya mwaka 1999.(MWANANCHI)