Thursday, July 11, 2013

SHIRIKISHO LA SOKA LAVIFUNGIA VILABU VILIVYOFUNGANA 79-0.

Shirikisho la soka nchini Nigeria limevifungia vilabu vinne baada ya kuandikisha matokeo ya kushangaza katika michuano ya kupanda daraja.

Vilabu hivyo ni pamoja na Plateau United Feeders FC, Akurba FC, Police FC na Bubayuaro FC.
 
Plateua United Feeders iliichabanga Akurba FC mabao 79 kwa 0 huku Police Machine FC ikaikagaraza Bubayaro FC mabao 67 kwa 0.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi katika chama cha soka nchini humo NFF Muke Umeh,amesema kuwa matokeo hayakubaliki kamwe na lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini vipi mabao hayo yalifungwa.
 
Plateau United na Police Machine FC walicheza mchuano huo wakiwa na alama sawa na mshindi alihitajika kupata mabao mengi li kujihakikishia kusonga mbele ili kupanda daraja na kucheza ligi ya Kitaifa.
 
Plateua United Feeders walipata mabao 72 katika kipindi cha pili cha mchuano wao huku, huku Police wakiandikisha mabao 61 katika kipindi cha kwanza cha mchuano wao.
 
Uongozi wa soka nchini Nigeria unasema kuwa hauwezi kueleza kilichitokea na wale wote watakaobainika kusababsiha matokeo hayo watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za soka nchini humo.

ALIYEFARIKI SIKU YA HARUSI YAKE AZIKWA NA MWANAE.

ROMBO, Ilikuwa ni majonzi, vilio na huzuni katika kijiji cha Mahalu, wilayani Rombo, Kilimanjaro kufuatia mazishi ya aliyetarajiwa kufunga ndoa Jumamosi marehemu Levina Swai pamoja na mwanawe.
Marehemu Levina alizikwa na mwanaye kaburi moja baada ya kichanga hicho kufariki siku hiyo hiyo mara baada ya mama yake kupoteza maisha kwa kile kilichodaiwa ni kuugua Malaria, shinikizo la damu kuwa chini na upungufu wa damu.
Marehemu Levina alifariki wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika kijiji cha Mahalu kata ya Makiidiwilayani Rombo, alikozikwa,wifi wa marehemu, Hortensia Mrima alisema wifi yake alifia hospitalini na alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi akiwa katika mpango wa ajira ya walimu wapya.
“Mimi ndiye nilikuwa namuuguuza hospitalini tangu Alhamisi iliyopita na alikuwa anasumbuliwa na malaria na kupungukiwa na damu na pressure (shinikizo la damu) kuwa chini,”alisema Mrima.
Ibada ya mazishi ilianza saa 8:30 mchana ikiongozwa na Padri Emmanuel Mavengero na kuhudhuriwa na waombolezaji kutoka Tanga na Kilimanjaro.
Mazishi hayo yalitawaliwa na simanzi huku waombolezaji wengi akiwamo aliyetarajiwa kumuoa marehemu Levina,Gabriel Swai muda wote alikuwa akibubujikwa na machozi na kushindwa kuzungumza.
Wifi huyo alieleza kuwa wifi yake alipopimwa alikutwa na Malaria 13 na kupewa dawa za malaria za SP na dripu za Quinine ambazo zilimlewesha sana na kuendelea kudhoofu.
“Siku hiyo ya Alhamisi alikata kauli akawa haongei ikabidi daktari amwekee dripu za Glucose ili kumuongezea nguvu na shinikizo la damu ilirudi sawasawa lakini bado alikuwa amelegea na alikuwa haongei,”alisema.
Ilipofika Jumamosi ambayo ndiyo siku iliyokuwa imepangwa kufunga ndoa na Gabriel Swai, ikabidi madaktari wamuwekee maji ya uchungu ili kumuokoa mtoto baada ya mama kuwa mahututi.
“Yale maji ya uchungu yalimsaidia akaweza kujifungua mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo 1.7 na baada ya kujifungua alipoteza fahamu na saa 8:05 mchana akafariki dunia,”alisema.
Kwa mujibu wa Mrima, mtoto aliendelea kuishi huku akipewa maziwa lakini alikuwa akiyatapika, hadi ilipofika saa 5:00 usiku alifariki dunia.