Wednesday, January 23, 2013

UHABA WA MADAKTARI BINGWA WAIKUMBA MUHIMBILI

DAR ES SALAAM-TANZANIA,

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inakabiliwa na upungufu wa madaktari  bingwa wa upasuaji, hususan katika kitengo cha watoto wanaougua maradhi ya saratani (cancer surgeons).

Upungufu huo unaelezwa umetokana na baadhi ya madaktari bingwa waliokuwapo awali kufariki dunia mwaka jana, baadhi kuacha kazi na wengine kustaafu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini madaktari bingwa wawili walifariki dunia mwaka jana, ambao ni Dk. Enock Sayi na Dk. Profesa Primo Carneiro, wakati Dk. Catherine Mng’ong’o anaelezwa kuacha kazi, huku Dk. Petronella Ngiloi akistaafu kwa mujibu wa sheria.
Habari zilizopatikana hospitalini hapo na kuthibitishwa na mamlaka husika, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinasema mbali na hospitali hiyo Kuu ya Taifa kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa, inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa mashine za oksijeni za kisasa za ukutani.

Mashine za oksijeni zilizopo zinadaiwa kufanya kazi chini ya kiwango kinachotakiwa.
Lakini msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja,  pamoja na kukiri kuwapo kwa upungufu huo wa madaktari bingwa, amesema hilo haliwezi kuathiri shughuli za tiba katika kitengo hicho cha magonjwa ya watoto.
Aidha, anasema hospitali hiyo imesheheni vifaa vya kisasa, zikiwamo mashine hizo za oksijeni, zinazotumika kumsaidia mgonjwa kupumua.

Uchuguzi uliofanywa na gazeti hili katika Jengo la Watoto na kwenye baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini pia kuwapo kwa vichwa vya mashine za mitungi ya oksijeni vikiwa vimezungushiwa plasta kuzuia uvujaji hovyo wa hewa hiyo, hali inayohatarisha afya za wagonjwa wanaolazwa katika wodi zenye mashine hizo.
“Hayo mambo yanashughulikiwa na Bodi ya Muhimbili pamoja na Mkurugenzi wake. Kama masuala hayo unayouliza yatahitajika kufika wizarani, ndipo hapo na sisi tunaweza kutolea ufafanuzi, lakini ninavyojua Muhimbili kuna vifaa vyote vya kisasa na ndiyo maana imeitwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili,” alisema  Mwamwaja.

Mmoja wa madaktari bingwa wa Muhimbili, ameliambia gazeti hili kwamba tangu walipofariki madaktari bingwa wenzake; Dk. Sayi na Profesa Carneiro mwaka jana, nafasi zao hadi sasa hazijajazwa.
Aidha, daktari bingwa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa sababu zilizo wazi kabisa, amethibitisha kuwapo kwa tatizo la madaktari bingwa katika kitengo cha saratani, baada ya Dk.  Ngiloi kustaafu.

Alisema awali baada ya Dk. Ngiloi kustaafu, Dk. aliyechukua nafasi yake hiyo katika kitengo hicho  alikuwa Dk. Mng’ong’o, lakini kwa sasa anadaiwa kuacha kazi hospitalini hapo.

BARAZA LA USALAMA LAONGEZA VIKWAZO KWA KOREA KASKAZINI

PYONG YANG-KOREA KASKAZINI,
Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa UN limeagiza kuwekwa kwa vikwazo zaidi dhidi ya Serikali ya Korea Kaskazini kufuatia nchi hiyo kuendelea kukaidi maazimio ya baraza hilo kuhusu kurusha maroketi wanayodai ni ya kisayansi.
Kwenye vikwazo hivyo vipya baraza hilo limeiongeza mamlaka ya anga ya nchi hiyo, benki, makampuni ya biashara na watu wanne ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali ya Pyongyang katika kutekeleza mpango wake wa kutengeneza roketi za masafa marefu.

Mapendekezo hayo ambayo yaliwasilishwa na nchi ya Marekani, yalipitishwa bila kupingwa na nchi wanachama 15 wa kudumu wa baraza hilo na kulaani kile ambacho imekiita ni ukaidi wa taifa hilo.

Mwezi Desemba mwaka jana nchi ya Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya kombora lake la masafa marefu kuelekea angani, jaribi ambalo yenyewe imesisitiza halihusiani na utengenezaji wa silaha za masafa marefu kama inavyodaiwa na nchi za magharibi.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo Suzan Rice amelitaka baraza hilo kuchukua hatua zaidi iwapo nchi ya Korea Kaskazini itaendelea kukaidi maazimio ya Umoja huo.

Nchi za Marekani na China zimekuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Serikali ya Pyongyang katika kujaribu kuishawishi nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kutengeneza makombora ya masafa marefu.

Licha ya vikwazo hivyo Serikali ya Pyongyang imeapa kuendelea na majaribio yake na kwamba hivi karibuni itateeleza jaribio jingine la roketi.

LULU AIOMBA MAHAKAMA IMWACHIE HURU.


DAR ES SALAAM- TANZANIA,
 MSANII wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imwachie huru kwa dhamana.

Lulu kupitia kwa wakili wake aliwasilisha ombi hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na Ijumaa jaji anayeisikiliza kesi hiyo anatarajia kutoa uamuzi.


Tangu kilipotokea kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba, Aprili 7, mwaka jana Lulu amekuwa akisota mahabusu na dhamana yake ikawa imezuiwa kwa mujibu wa kesi za mauaji.

Hata hivyo baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia hivyo kumuweka katika mazingira ya kupatiwa dhamana. Habari zilizopatikana mahakamani hapo jana zilisema kuwa tayari maombi hayo ya dhamana yamepangwa kusikilizwa na Jaji Zainabu Muruke, Januari 25 ,2013.


Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake linadhaminika.


Katika hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona yanafaa.

Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama hii tukufu.”

Alidai kuwa akiwa wakili wa mwombaji, anatambua kuwa mwombaji anao wadhamini wa kuaminika ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.

Wakili Kibatala katika hati yake hiyo ya kiapo anadai kuwa akiwa wakili wa mshtakiwa, ikiwa mshtakiwa huyo atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.

Aliendelea kudai kwamba kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo amepata fursa kubwa ya kufahamiana na mwombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo anajua kuwa mwombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.


“Mwombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake ambao wako tayari kuhakikisha kuwa anatimiza masharti na kuhakikisha kuwa anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote’, alisema.

“Mwombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam na hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa masharti yoyote ya dhamana,” anasisitiza Wakili Kibatala na kuongeza: