Wednesday, October 31, 2012

KIMBUNGA CHA SANDY CHASABABISHA HASARA ZAIDI YA DOLA BILIONI ISHIRINI.




MAREKANI,
Rais wa Marekani Barack Obama atangaza majimbo ya kaskazini mashariki ya Marekani ya New York na New Jersy kuwa maeneo ya "maafa makubwa" baaada ya kimbunga kikubwa kilichopewa jina la Sandy.

Tangazo hilo limetolewa hapo jana siku ya jumanne na linaruhusu kutumika kwa fedha ya serikali katika maafa hayo.

Kimbunga Sandy kilifika nchi kavu siku ya Jumatatu jioni na kinaendelea kupunguka nguvu zake kinapita sehemu za kati na kaskazini ya marekani. Maafisa wanasema watu 16 walifariki katika katika maeneo ya mashariki ya Marekani kutokana na kimbunga hicho ambacho kilisababisha vifo vya watu 65 wiki iliyopita katika nchi za Caribbean.

Kwa siku ya pili mfululizo shughuli zote za serikali na biashara pamoja na shule katika miji mikubwa mashariki ya Marekani ziliendelea kufungwa siku ya Jumanne wakati mamilioni ya watu wakiwa hawana huduma ya umeme.

Takriban wasafiri elfu 10 walikwama katika miji hiyo ya mashariki ya nchi baada ya maelfu ya safari za ndege kuahirishwa kwa siku ya pili. Halikadhalika huduma za usafiri wa mijini iliendelea kufungwa na mjini New York kumekuwepo na mafuriko ya maji katika njia za reli za chini kwa chini.

Watalamu wa uchumi wanatabiri kwamba kimbunga Sandy huwenda kimesababisha hasara inayogharimu takriban dola bilioni 20.(VOA)

CHELSEA YAMTUHUMU MWAMUZI DHIDI YA MATAMSHI YA KIBAGUZI KWA MIKEL OBBI




LONDON-UINGEREZA,
Klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza imemtuhumu mwamuzi aliyechezesha wa mchezo wao na Manchester United Mark Clattenburg kumtolea maneno ya kibaguzi kuungo wake raia wa Nigeria John Mikel Obi. Msemaji wa Chelsea ameweka bayana wameshawasilisha malalamiko yao ili hatua zichukuliwe dhidi ya Clattenburg ambaye amekumbana na ukosoaji mkubwa kwa kile kinachoelezwa ni kushindwa kuumudu mchezo huo. Chama cha Waamuzi wa Kulipwa PGMO kimekiri kupokea malalamiko hayo na kusema watayafanyia kazi kwa kadri ambavyo itaonekana na uchunguzi utafanyika ili kubaini iwapo Clatternburg alitoa maneno ya kibaguzi kwa Mikel Obi. Katika mchezo huo Manchester United ilivunja mwiko wa kushindwa kupata ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu katika uwanja wa Stamford Bridge kwa kipindi cha miaka kumi baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-2. Chelsea ililazimika kumaliza ikiwa na wachezaji tisa baada ya kushuhudia Branislav Ivanovic na Fernando Torres wakilimwa kadi nyekundu kitu ambacho kilizusha lawama za kila mara kwa mwamuzi Clattenburg. Manchester United ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata goli kupitia kwa David Luiz ambaye wakati anaokoa akaukwamisha mpira wavuni kabla ya Robin Van Persie kufunga goli la pili na kushuhudia Juan Mata akifunga goli la Chelsea kabla ya mapumziko. Kipindi cha pili Chelsea waliongeza kasi na kufanikiwa kupata goli la kusawazisha kupitia Ramires kabla ya Javier Hernandez hajafunga goli la tatu na la ushindi dakika kumi na tano kabla ya mchezo kumalizika na kuiba ushindi Manchester. Goli la Hernandez lilizidisha hasira kwa wachezaji wa Chelsea na hata mashambiki wake kutokana na kudai mfungaji alikuwa kwenye eneo la kuotea na halikustahili kuwa goli na kushuhudia Mikel Obi akilimwa kadi ya njano kwenye malumbano hayo. Kwa matokeo hayo sasa Chelsea inaendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi moja baina yake na Manchester United ambayo imepiteza michezo mieili tangu kuanza kwa Ligi msimu huu na huu ukiwa mchezo wa kwanza kwa The Blues kufungwa.(Chanzo RFI)