Tuesday, August 21, 2012

MAHAKAMA KUU TABORA YATENGUA USHINDI WA DK.KAFUMU.

http://t3.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcQWhv8Qn16oTZNOCpQyMoURwHU0PzoCSKDF4AhDMk-ahQApWNq1aw&t=1TABORA-TANZANIA,
Mahakama kuu Kanda ya Tabora imetengua rasmi matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa kiti cha ubunge mgombea na aliyekuwa Mbunge wa Igunga kupitia chama cha Mapinduzi(CCM) Dk Peter Kafumu, katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana. 

Hukumu hiyo imefuatia kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea katika uchaguzi huo kupitia tiketi ya chama cha demokrasia na Maendeleo Profesa Abdalla Safari  aliyemshitaki mgombea, huyo, mwanasheria mkuu wa Serukali, na msimaizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Katika kesi hiyo hoja mbalimbali zilitolewa kupinga matokeo hayo ikiwemo ya  matumizi mabaya ya madaraka kwa Waziri wa Ujenzi John Magufuli kufanya mkutano wa kampeni Kata ya Igulubi wilayani Igunga na kuahidi ujenzi wa Daraja la Mbutu kama wananchi hao watampigia kura mgombea wa chama mapinduzi na kuwatisha wananchi kuwa wasipoichagua CCM watashughulikiwa.

Katika hoja nyingine mgombea huyo kupitia tiketi ya  CHADEMA akiwakilishwa na wakili wake walimshitaki Rais mstaafu Benjamini Mkapa aliyetoa ahadi kwa wananchi wa Igunga siku moja kabla ya Uchaguzi, pamoja na ile ya baraza la Waislamu (Bakwata) wilaya ya Igunga kuwakataza waumini wake wasikipigie kura chama cha CHADEMA.
 

WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA AFARIKI DUNIA

 



ADDIS ABABA-ETHIOPIA
 Waziri mkuu wa Ethiopia Bw.Meles Zenawi, 57 amefariki dunia huku Brussels Ubelgiji usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taarifa za kifo cha waziri mkuu huyo zimetangazwa na msemaji wake Bw.
 Bereket Simon amesema waziri huyo alifariki katikati ya usiku baada ya kukimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi.Kifo cha waziri mkuu huyo kilizushwa kwa muda mrefu na hali ikawa ya wasiwasi zaidi baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Africa mwezi uliopita.

Makamu waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Hailemariam Desalegn ataapishwa punde kushika wadhifa huo mpaka chama tawala kitakapomchagua mrithi wa Bw,Zenawi kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

 Umoja wa Afrika umetuma salamu zake za rambi rambi kwa Ethiopia na kuelezea kifo hicho kama pigo kubwa kwa Afrika iliyompoteza mtoto Mahiri na hodari.

Uingereza pia kupitia kwa waziri Mkuu Bw.David Cameron imeelezwa kuguswa na msiba huo ikimtaja Waziri huyo kama mmoja ya Wazungumzaji wenye ushawishi barani Afrika.
Meles aliingia madarakani mwaka 1991 akimbadili Haile Mariam aliyekuwa kiongozi wa kijeshi na alisifiwa na wengi kwa juhudi zake zilizosaidia kukua haraka kwa uchumi wa nchi hiyo masikini.

Licha ya kulaumiwa na makundi ya haki za binadamu nchini humo kwa wakati fulani, waziri huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa jirani zake Somalia hasa katika mapambano dhidi ya
waasi pamoja na makundi yanayoshirikiana na Al Qaeda hali iliyomfanya rafiki mkubwa pia wa nchi za Magharibi. 
Hata hivyo haijawekwa wazi wapi na siku gani waziri huyo atazikwa.

MGODI ULIOUA AFRIKA KUSINI WAHAIRISHA TISHIO LA KUWAFUKUZA KAZI WAFANYAKAZI WALIOGOMA.

 http://www.globalpost.com/sites/default/files/imagecache/gp3_slideshow_large/south_africa_lonmin_marikana_miners_fired_20120820.jpg
 MARIKANA-AFRIKA KUSINI,
Uamuzi wa kuwafukuza wafanyakazi waliogoma  kushinikiza kuongezwa kwa mishahara na kupinga mauaji ya wenzao katika mgodi wa Marikana nchini Afrika kusini umegonga mwamba baada ya kampuni ya Lonmin inayomiliki mgodi  kuondoa tishio hilo.Akitangaza uamuzi huo makamu rais wa kampuni hiyo Bw.Mark Munroe amesema kuwafukuza maelfu ya wafanyakazi hakutasaidia kitu na hivyo kampuni yao imeamua kuondoa tishio hilo.

Ni asilimia 33 tu ya wafanyakazi 28,000 waliokuwa wameripoti kazini mpaka leo Jumanne ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho waliopewa na mgodi huo kurudi kazini, huku asilimia 67 ya wafanyakazi wakiwa bado wamegoma hali iliyoulazimu mgodi huo kusalimu amri.
Wafanyakazi hao wapo katika mgomo kushinikiza kuongezwa kwa mishahara yao na pia wakiwa katika maombolezo ya vifo vya wenzao 34 waliopigwa risasi katika mapambano na polisi wiki iliyopita.

Serikali ya Afrika kusini imeutaka mgodi huo kuachana na uamuzi huo na kusubiri kutafutwa kwa suluhu nyingine ambayo itakuwa na msaada kwa tatizo hilo.
  Wakati huo huo Bunge la Afrika kusini ambalo litakaa siku chache zijazo pamoja na mabo mengine litajadili suala hilo na kulitolea uamuzi, viongozi wa kisiasa wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama vya siasa wameutembelea mgodi huo kujionea hali halisi ikiwa ni maandalizi ya mjadala unaotarajiwa kuwa mkali kuhusu tukio hilo.