Monday, July 08, 2013

Murray bingwa mpya wa Wimbledon

Andy Murray

Andy Murray amekuwa Muingereza wa kwanza kushinda taji la Wimbledon tangu mwaka 1936, ikiwa ni zaidi ya miaka 77.

Murray amemfunga Novak Djokovic raia wa Serbia kwa seti tatu kwa kwa bila katika mchezo wa fainal za wanaume za michuano ya tenesi ya Wimbledon.

Murray amemshinda mchezaji anayeorodheshwa wa kwanza duniani Novak Djokovic kwa seti tatu kwa bila za 6-4, 7-5, 6-4.

Andy Murray amesema anashindwa kuamini kile alichokifanya kwani mechi hiyo ilikuwa ngumu, huku joto likiwa kubwa lakini anashukuru ameweza kumaliza mechi hiyo kwa ushindi muhimu kwake na kwa taifa.

Hili ni taji la pili la michuano mikubwa ya tenesi duniani maarufu kama Grand Slam baada ya kushinda lile la Michuano ya wazi ya Marekani.

Muingereza wa mwisho kushinda taji la Wimbeldon ambalo hufanyika mjini London kila mwaka alikuwa ni Fred Perry aliyeshinda taji hilo kwenye michuano ya mwaka 1936.

Mwaka jana Andy Murray alipoteza mchezo wa fainali ya michuano ya Wimbledon kwa kufungwa na Roger Federer.

Malkia wa Uingereza, Elizabeth wa pili amemtumia ujumbe wa Pongezi Andy Murray kwa ushindi wake katika mechi ambayo ilishudiwa pia na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon

Nyati mweupe azua tafrani Ngorongoro

WAHIFADHI watafiti na wataalamu kadhaa, wako katika harakati za kumsaka Nyati wa ajabu anayedaiwa kuwa na rangi ya maziwa, ambaye hivi karibuni ameonekana katika mwambao wa bonde kuu la Ngorongoro (Kreta) na kusababisha tafrani kubwa.

Kwa mujibu wa mtalaam wa ikolojia katika mamlaka hiyo, Patrice Mattay, uwepo wa nyati (mbogo) huyo wa aina yake hifadhini hapo, kumeibua suala jipya katika utafiti wa wanyama pori, kwani hakujawahi kuwepo Nyati mwenye rangi nyeupe popote duniani. Kwa kawaida Nyati huwa anangozi yenye rangi nyeusi.

Nyati huyo mweupe aligundulika kwa mara ya kwanza na maafisa wa polisi wanaofanya kazi katika kituo cha polisi kilichopo ndani ya hifadhi hiyo, ambao wanasema mnyama huyo hupita katika maeneo ya kituo hicho majira ya asubuhi akiwa miongoni mwa mbogo wengine takribani 20. Ngorongoro ina nyati wapatao 350.

“Ni kweli hata mimi binafsi nimemshuhudia Nyati huyo mweupe akikatiza katika sehemu mbalimbali za hifadhi ya Ngorongoro majira ya asubuhi akiwa katika kundi la mbogo wengine,” alisema mkuu wa kituo cha Ngorongoro Afisa wa Polisi, JJ Paul.

Hadi sasa ni maaskari wanaofanya doria katika maeneo ya hifadhi hiyo, hususan nyakati za asubuhi, ndio wanaothibitisha kwa kiwango kikubwa kumuona Nyati huyo wa ajabu ambaye sasa anatarajiwa kuwa atakuwa kivutio kipya cha utalii nchini.

Meneja Uhifadhi katika mamlaka ya Ngorongoro, Amiyo T. Amiyo amesema tayari shirika lake limekwisha tuma askari wake kadhaa kumsaka Nyati huyo wa ajabu, ili kubaini eneo ambalo anapatikana kwa ajili ya kuwezesha utafiti zaidi.

“Na kwa mtu yeyote mwenye kutuletea taarifa kuhusu Nyati huyo mweupe zitakazotuwezesha kumpata mnyama huyo, basi naye pia atazawadiwa ipasavyo,” alisema Amiyo.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndiyo inayoongoza kwa kupata watalii wengi nchini na kwa mujibu wa Ofisa Utalii wa Shirika hilo, Asantaeli Melita, zaidi ya wageni 585,000 hutembelea eneo hilo, na hasa Kreta, kila mwaka.

Idadi ya wanyamapori walioko Ngorongoro kwa sasa inafikia 300,000 wengi wao wakiwa ndani ya bonde lenyewe huku baadhi na hasa twiga wakiishi nje ya Kreta.

Mbali na Mbogo wa jabu aliyegunduliwa hivi karibuni, eneo la Ngorongoro pia lina maajabu mengine kadhaa, ukiwemo kilima cha mchanga unaotembea bila kusambaratika, idadi kubwa ya Kakakuona, mnyama anayedaiwa kuwa na uwezo wa kutabiri, pamoja na idadi kubwa ya wanyama adimu kama Mbwa-mwitu na Faru.

USAFIRI DAR KITENDAWILI

DAR ES SALAAM, Abiria  waliokuwa wasafiri kwenda mikoani na nchi jirani, wamekwama katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo kutokana na uchache wa mabasi.

Mwananchi jana ilishuhudia mamia ya abiria wakisubiri mabasi yalikuwa njiani  kurejea Dar es Salaam ili na wao waweze kusafiri kwa mabasi hayo.

Katika kituo hicho ambacho kwa kawaida huwa na mabasi mengi, kwa siku ya jana muda wa saa nne hadi tano ni mabasi matatu tu ya Shabiby Line, Hood na Simba One ndio yalikuwa yakipakia abiria kuelekea Morogoro na Dodoma,huku kukiwa hakuna basi lolote la kuelekea mikoa ya Kaskazini.

Abiria hao wengi wakiwa ni wanafunzi walikuwa wakirejea shuleni kwa ajili ya muhula mpya wa masomo unaotarajiwa kuanza leo.

Wakizungumza na Mwananchi walisema wanadhani uhaba wa mabasi umetokana na uwapo wa wanafunzi wengi ambao wanarudi shule baada ya kumaliza likizo za katikati ya mwaka.

“Sisi tumekata tiketi tangu jana ya kwenda Dodoma, tunakwenda Msalato Sekondari,lakini leo tumefika hapa asubuhi na tulitakiwa kuondoka na basi la saa nne lakini mpaka saa tano hii tunaambiwa tusubiri basi liko njiani linakuja”walisema wanafunzi ambao hawakutaka kutaja majina.(MWANANCHI)