Wednesday, March 06, 2013

UCHAGUZI KENYA-MITAMBO YALETA KIZAA ZAA, KENYATTA BADO ANAONGOZA

Kenyan authorities are trying to guard against fraud and violence when they hold a presidential election on March 4. Here, voters register on biometric equipment last December in Nairobi. (Image credit: AFP/Getty Images)NAIROBI-KENYA,
Kufikia sasa asilimia 42 ya kura za urais nchini Kenya zimehesabiwa na kuwasilishwa rasmi kwa tume ya uchaguzi IEBC kupitia mitambo ya electroniki.
Hata hivyo kumekuwepo malalamishi kuhusu kucheleweshwa kwa shughuli ya kujumlisha kura kutokana na hitilafu ya mitambo.

Uhuru Kenyatta, anayekabiliwa na kesi katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC, angali anashikilia uongozi huku kura za urais zikiwa bado zinahesabiwa.Huu ni uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika tangu ghasia za baada ya mwaka 2007/2008 kufuatia matokeo yaliyozua utata.

Kenya iliendelea kuwa mbele kwa hesabu ya matokeo ya mwanzo dhidi ya mpinzani wake waziri mkuu Raila Odinga katika siku ya pili ya shughuli ya kuhesabu kura zaidi ya masaa 36 baada ya shughili ya upigaji kura kukamilika.

Raila Odinga alidai kuibiwa ushindi wake mwaka 2007 wakati matokeo yalizua ghasia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki moja huku maelfu wakiachwa bila makao.

Wakati mamilioni ya wakenya walijitokeza kupiga kura kwa amani siku ya Jumatatu,watavyopokea matokeo ya mwisho ya kura ndio itakuwa ishara ya uthabiti wa nchi hiyo.

Ni asilimia arobaini na moja ya kura zilizohesabiwa huku kukiwa na vituo zaidi ya elfu thelathini ambako kura zilipigiwa.
Ni zaidi ya kura milioni tano zilizohesabiwa kutoka kwa wapiga kura milioni 14.3 waliokuwa wamesajiliwa.

RAIS WA VENEZUELA HUGO CHAVEZ AFARIKI DUNIA

 
CARACAS-VENEZUELA,
Katika taarifa kwa taifa, makamu wa rais wa Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez ametoweka katika hadhira ya nchi hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa mara ya kwanza tangu maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali ya kijeshi kuendelea kupokea matibau. Hata hivyo maelezo zaidi hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu  mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao.
Bwana Chavez amekua uongozini nchini Venezuela kwa miaka 14 na anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha ya raia wa pato la chini.

Ujumbe wa Jeshi

Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa wataendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.

Wasifuwa Chavez

Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini.

Chavez na jamii ya kimataifa
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.