Tuesday, March 26, 2013

ZAIDI YA WANAFUNZI 4,800 HAWAJUI KUSOMA NJOMBE

NJOMBE-TANZANIA,
ZAIDI ya wanafunzi 4,800 wa darasa la nne hadi la saba, katika shule za msingi mkoani Njombe hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu. Hayo yalielezwa na Ofisa Elimu Takwimu mkoani hapa, Sandagila Mgaya, alipotoa taarifa ya elimu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na watendaji mbalimbali wa mkoa, Mgaya alisema hali hiyo ni mbaya na inahatarisha maendeleo ya elimu katika mkoa huo mpya.

Alisema kati ya wanafunzi hao wasiojua kusoma, kuhesabu wala kuandika, wapo 19 wanaosoma kidato cha pili na tatu katika shule za sekondari katika mkoa huo.

Utafiti uliofanywa umebainisha kuwa idadi ya wanafunzi hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu imeongezeka jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu katika mkoa huo, alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi alikiri kuwa hali ya elimu mkoani humo ni mbaya na kuwataka wadau wa kikao hicho kujadili uwezekano wa kutatua tatizo hilo.

Alisema lazima kuhakikisha mkoa huo unapata njia ya kuwasaidia wanafunzi hao waweze kusoma, kuandika na kuhesabu ili kukuza kiwango cha elimu mkoani.

“Hali ya elimu ni mbaya kwa matokeo ya kidato cha nne mpaka cha sita, lakini cha ajabu zaidi wapo wanafunzi wengi wa darala la nne hadi la saba, ambao hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu jambo ambalo ni hatari,” alisema.

Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Philemon Luhanjo, aliutaka mkoa huo kutilia mkazo elimu ya watu wazima kuwapa elimu ya stadi za maisha wanafunzi wanaomaliza bila kujua kusoma, kuhesabu na kuandika.

Wakichangia katika kikao hicho baadhi ya wadau wa elimu walisema kutojua kusoma, kuandika na kuhesabau kwa wanafunzi hao kunasababishwa na baadhi ya shule kutokuwa na walimu wa kutosha.

Waliitaka Serikali kupunguza idadi ya masomo kwa wanafunzi wa awali, darasa la kwanza na la pili ili watiliwe mkazo kusoma, kuandika na kuhesabu peke yake.

Suala la kushuka kiwango cha elimu nchini limekuwa gumzo kubwa nchini hivi sasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walishindwa.

Jambo hilo liliibua mjadala mzito katika kikao cha Bunge kilichopita, hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi ambayo pamoja na mambo mengine alitaka iundwe kamati ya bunge kuchunguza mfumo mzima wa elimu nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekwisha kuunda tume inayochunguza kushindwa kwa kiwango kikubwa kiasi hicho kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana

MAJESHI YA KOREA KASKAZINI YAJIWEKA TAYARI KUSHAMBULIA KUSHAMBULIA KAMBI ZA JESHI LA MAREKANI MJINI HAWAI NA GUAM.

 

PYONGYANG-KOREA KASKAZINI,
Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuviweka tayari vikosi vyake kwenye mstari wa mapambano tayari kwa mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani za mjini Hawaii na Guam pamoja na Kora Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa shirika la utangazaji wa Korea Kaskazini, imesema kuwa amri imetolewa na kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo ambayo inawataka wanajeshi wote kuwa mstari wa mbele tayari kwa kusubiri amri ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani.


Tangazo hilo la Serikali ya Korea Kaskazini linakuja wakati ambapo nchi ya Korea Kusini na Marekani zimemaliza mazoezi ya pamoja ya kijeshi ambayo Korea Kaskazini ilidai kuwa ni uchokozi dhidi ya taifa lao.


Hii si mara ya kwanza kwa Korea Kaskazini kutangaza kutishia kuishambulia nchi ya Marekani ambapo imeapa kutumia silaha za Nyuklia kutekeleza mashambulizi yake dhidi ya maadui zake.

Picha za video zimemuonesha kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un akitembelea kambi za wanajeshi wa nchi hiyo ambao wamekuwa kwenye mazoezi ya kijeshi kujiweka tayari kuilinda nchi yao.