Friday, March 15, 2013

PAPA FRANCIS AFANYA MAAJABU KATIKA SIKU YAKE YA KWANZA.

 

VATCAN-ITALIA,
PAPA Francis I ameonesha maajabu katika siku yake ya kwanza ya upapa, baada ya jana kwenda katika hoteli aliyofikia kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa wa 266 katika historia ya Kanisa Katoliki duniani, kuchukua mizigo yake na kulipa bili yeye mwenyewe.

Hali hiyo, iliashiria kuachana na staili za watangulizi wake, ambao wamezoea kufanyiwa shughuli kama hizo na watumishi wao, huku wenyewe wakijifungia ndani ya nyumba za gharama ambazo kuta zake zimenakishiwa kwa dhahabu za mjini Vatican.

Jambo la pili ambalo lilionekana kuwavutia wengi, ni pale alipoachana tena na desturi za mapapa waliopita, uchaguzi wa mavazi ya kipapa ya Francis I ulijidhihirisha kwa kuvalia vazi la kawaida lisilotofautiana na lile la zama zake za uaskofu.

Askofu huyo wa zamani wa Buenos Aires, Argentina, Kardinali Jorge Bergoglio, alianza siku yake ya kwanza kwa kufanya ziara kwa kutumia gari la kawaida la Vatican kuelekea Basilica la Roman ili kufanya maombi kwa Bikira Maria, akilenga kulileta kanisa karibu na watu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, alihudhuria misa ya maombi katika Kanisa la Santa Maria Maggiore mjini Roma, ili kuanza kazi yake kama mkuu wa Wakatoliki bilioni 1.2 kote duniani.

Papa huyo wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, alipokea ujumbe na salamu mbalimbali kutoka duniani kote kumtakia heri.

Miongoni mwao, ni Rais wa Marekani, Barack Obama, aliyemtaja Bergoglio kuwa mtetezi wa masikini na wanyonge, huku Makamu wake, Joe Biden akitarajia kuongoza ujumbe wa nchi hiyo katika sherehe za kumsimika zitakazofanyika Jumanne wiki ijayo.

Aidha Waziri Mkuu wa Australia, Julia Gillard, alisema kuchaguliwa Papa kutoka ‘ulimwengu mpya’ ni tukio ambalo lina umuhimu wa kihistoria.

Viongozi wengine, waliotuma pongezi ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Rais wa Argentina, Cristina Kirchner.

Francis, ambaye ndiye Papa wa kwanza asiyetoka Ulaya katika kipindi cha takribani miaka 1,300, aliitumia ibada yake ya kwanza kumwombea mtangulizi wake, Benedict VXI na kutoa wito wa kuwepo udugu miongoni mwa waumini wa Kikatoliki.

Lakini Muargentina huyo, pia anakabiliwa na mlolongo wa changamoto ngumu zinazolikabili kanisa hilo.

Kanisa hilo, limekumbwa na migawanyiko mikubwa ya ndani na kashfa zilizowakumba makasisi za kuwadhalilisha watoto kingono na tuhuma za ufisadi na kuvuja kwa nyaraka za siri.

Awali alikuwa ameuambia umati wa watu 100,000 uliofurika katika kiwanja cha Mtakatifu Petro kwamba amepanga kumwomba Bikira Maria ili auangalie mji mzima wa Rome.

Aliwaambia makardinali kwamba atamtembelea Papa mstaafu Benedict XVI, lakini Vatican ilisema ziara hiyo itafanyika siku chache zijazo.

Ratiba kuu ya Papa Francis I, jana ilikuwa kuzindua ibada ya jioni katika Kanisa dogo la Sistina, ambako makardinali juzi usiku walimchagua kuwa kiongozi wa kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2.

Anatarajia kutumia zaidi Kiitaliano na kuachana na utamaduni wa Benedict ambaye alijikita zaidi katika Kilatini.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76, anayesemekana kushika nafasi ya pili nyuma ya Papa Benedict XVI alipochaguliwa mwaka 2005, alichaguliwa katika raundi ya tano kumrithi papa huyo wa kwanza kujiuzulu kipindi cha miaka 600. Soma zaidi makala kuhusu Papa huyu mnyenyekevu ukurasa wa 26.

SILAHA AZUNGUMZIA KUKAMATWA KWA LWAKATARE


DAR ES SALAAM-TANZANIA,
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, ameibua madai mazito dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa, baada ya kudai kuna maofisa watatu wa ngazi za juu wa idara hiyo wanahusika na mipango ya kudhoofisha chama hicho.

Dk. Slaa, alisema maofisa hao, ambao aliwataja majina hadharani jana, ndio wanaodaiwa kupanga mikakati ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alidai mpango wa kukamatwa kwa Lwakatare uliandaliwa na maofisa watatu wa ngazi za juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.


Alisema mpaka sasa, chama hicho kimefanikiwa kupata majina ya maofisa hao ambao wanaaminika kupanga mikakati ya kutaka kudhoofisha mipango na maendeleo ya chama hicho.

Lwakatare alikamatwa juzi akihusishwa na tuhuma za kupanga mikakati mbalimbali ya kushambulia na kudhuru watu mbalimbali, wakiwamo waandishi wa habari.

Alisema mkakati wa kumkamata Lwakatare na wabunge wengine wa chama hicho, ulianza tangu mwaka jana, baada ya kuwapo na barua nyingi feki zilizokuwa zikibuniwa na kuonekana zimesainiwa na Lwakatare, Dk. Slaa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Nilipata taarifa Machi 11, mwaka huu kutoka kwa mmoja wa maofisa Usalama wa Taifa, Lwakatare atakamatwa, katika hili sasa imedhihirika kile tulichoambiwa na wasiri wetu ndicho kimetokea.

“Bahati nzuri gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), limesema Lwakatare anatuhumiwa kupanga njama za kumdhuru Mhariri wa gazeti hilo, na kwamba amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, sasa sisi hatujui walitoa taarifa hizo wapi.

“CHADEMA tunafurahia kama utaratibu huu, utafuata sheria na kuanika ukweli wa tukio hilo, kwani linafanana na kutekwa kwa Kibanda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka,” alisema Dk. Slaa.

“Chadema tunasema, aliyekuwa anamhoji Lwakatare akamatwe ili kila mtu amjue na picha zake zinazoonyeshwa kwenye mtandao ili kuondokana na upuuzi huu,” alisema.

“Mpaka sasa, Lwakatare bado anashikiliwa na polisi na hata chakula tulichopeleka asubuhi kimekataliwa kupokelewa…tunasisitiza tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kumpa dhamana pindi tutakaporuhusiwa.

“Tunarudia kusema mara zote, tumekuwa tukimshauri Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru ya uchunguzi, lakini ameendelea kuwa kimya, leo tunarudia kusema hatuna imani na tume za polisi kwani ni moja ya kundi linalohusishwa na matukio ya kuteka na kutesa.

“Tunapenda kuwaambia Watanzania na dunia nzima, CHADEMA hakina nia ya kuzuia polisi wasifanye kazi zao, tunataka wafuate sheria na taratibu zilizowekwa, katika hili la kutaka kutudhoofisha na kuminya uhuru wa vyombo vya habari hatutalivumilia liendelee.

“Tunasema ifike wakati propaganda za Serikali ziachwe na haki itendeke kwa manufaa ya taifa, itakumbukwa chama hiki na wanachama wake, kimekuwa kikisumbuliwa hata bungeni wabunge wameondolewa katika kamati na zingine kuvunjwa, bila kambi ya upinzani kuhusishwa,” alisema.

Pamoja na mambo mengi na historia ya matukio ya utekeji, kuuawa na kujeruhiwa, Dk. Slaa alimuomba Rais Kikwete kuwaeleza Watanzania juu ya kauli aliyoitoa Adis Ababa nchini Ethiopia, wakati wa mkutano wa Mpango wa Kujitathmini katika Utawala Bora (APRM) kwamba gazeti la Mwanahalisi lilifungiwa kutokana na kuandika habari za uchochezi.

Dk. Slaa, alimuomba Rais Kikwete kutumia mamlaka aliyonayo kulifungulia gazeti la Mwanahalisi, kwani ni haki ya kila Mtanzania kupata habari.

Vile vile alisema wakati umefika watuhumiwa wote waliotajwa katika matukio mbalimbali ya kuteka, kupiga, kujeruhiwa na kuua kuchukuliwa hatua katika vyombo vya sheria.

Lwakatare alikamatwa juzi na maofisa watatu wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupanga mikakati mbalimbali ya kudhuru watu, wakiwamo waandishi wa habari ambapo hadi jana, alikuwa akishikiliwa na polisi.

Hatua ya kushikiliwa Lwakatare, imekuja baada ya kuonekana kwenye CD iliyorekodiwa, akionekana akipanga mikakati hiyo.

Inadaiwa CD hiyo ilirekodiwa Desemba 28, mwaka jana na inaonekana kwa muda wa dakika saba tu.