Thursday, April 18, 2013

MANCHESTER UNITED YAZIDIWA THAMANI NA REAL MADRID


LONDON-UINGEREZA,
Manchester United wameondolewa kwenye nafasi ya kwanza ya klabu yenye utajiri na thamani kubwa inayotolewa na jarida la Forbes.

United wamekuwa wakishika nafasi ya kwanza kila mwaka tangu Forbes walipoanza kutoa list ya vilabu vye thamani kubwa zaidi duniani mwaka 2004, lakini mwaka huu wameondolewa kileleni na Real Madrid - klabu ambayo iliitoa kwenye michuano ya champions league hive karibuni.

Barcelona wanashika nafasi ya tatu nyuma ya United, Arsenal wapo nafasi ya nne na mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich wakikamilisha nafasi ya tano.

Real Madrid wanatajwa kuwa na thamani ya £2.15billion - na kwa namba hizo klabu hiyo ya Spain inakuwa ndio klabu ya michezo yenye thamani kubwa zaidi duniani - huku Manchester United wakiwa na thamani ya £2.07billion.

Kwa upande wa wachezaji wa soka, David Beckham bado anaongoza kwa utajiri akiwa ameingiza kiasi cha kati ya £33m - £29m ambazo zimetokana zaidi na mikataba ya kibiashara ya matangazo.

Staa wa Real Madrid Ronaldo ameingiza kiasi cha (£28.8m) akishika nafasi ya pili, wakati mwanasoka bora wa dunia Lionel Mess akishika nafasi ya 3 kwa kuingiza jumla ya £26m mwaka jana kwa kupitia mshahara na mikataba ya kibiashara.

HALI YATIBUKA BUNGENI-WABUNGE WATANO WATOLEWA NJE.



DODOMA-TANZANIA,
Wabunge watano wa Chadema jana walitimuliwa bungeni na kuamriwa kukaa nje ya Bunge kwa siku tano kutokana na vurugu zilizotokea jana usiku.


Wabunge hao ni Lissu, Hezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).


Chanzo za kufukuzwa kwao ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje Lissu ambaye alikuwa ameamriwa kutoka nje na Naibu Spika, Job Ndugai baada ya kuingilia hotuba ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba.


Kutokana na tafrani hiyo, Nchemba hakuweza kuhitimisha hotuba yake hivyo Ndugai alilazimika kukatisha mkutano wa Bunge.Hata hivyo wakati akiahirisha mkutano huo, tayari wabunge hao walikuwa wameshatolewa nje baada ya askari kuongezwa.


Mapema Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alitoa tusi zito la nguoni wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, licha ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kupiga mkwara wa kuwashughulikia wabunge watakaorusha matusi.


Mbali na tukio hilo Lema naye alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu viongozi wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa udini, madai ambayo Bunge limempa siku saba kuyathibitisha.


Lema aliituhumu CCM na Serikali yake chini ya Rais Kikwete kwa kushindwa kutatua mgogoro wa kidini na badala yake kuwa kama analikwepa tatizo. Alionya kuwa Taifa linapasuka kwa migogoro kutokana na viongozi wa Serikali kushindwa kulishughulikia.


Kauli iliwanyanyua vitini Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu na Sera), William Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Lukuvi na Jaji Werema walisimama wakidai kuwa Lema alikuwa amemdhihaki Rais Kikwete kwa kauli zake za kumhusisha na masuala ya udini.


Hata hivyo, Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Lissu alisimama kumtetea Lema akidai hakuwa amemdhihaki Rais bali alikuwa amemkosoa kitu ambacho kanuni za Bunge zinaruhusu.


Lema aliruhusiwa kuendelea na hoja yake na ndipo akamtolea mfano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira wakati alipokwenda Mwanza kutatua mgogoro baina ya Wakristo na Waislamu kuhusu suala la kuchinja.


“Wassira akifahamu yeye ndiye, Waziri alikwenda Mwanza na kuwaacha viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu watatue wenyewe suala la kuchinja. Sasa alitaka diwani atatue mgogoro ule?”


Baada ya kumaliza kuchangia, Naibu Spika alitangaza kuwa Lema anatakiwa kuwasilisha katika muda wa siku saba uthibitisho kuwa Rais anahusika na tatizo la udini.(MWANANCHI)