Wednesday, January 09, 2013

baadhi ya Wajumbe wa Umoja wa Mataifa waunga mkono kutumika kwa ndege za upelelelezi Congo.



Waasi wa M23 wanaohatarisha usalama wa Mashariki mwa Congo

DRC CONGO,
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,UN wameunga mkono pendekezo la kuanza kutumika kwa Ndege maalum za upelelezi mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC ili kulinda usalama wa Raia.

 Mkuu wa Operesheni za Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous amesema kuwa amewasilisha ombi maalumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha mpango wa kutumika kwa ndege maalumu zenye uwezo wa kuona hata wakati wa usiku kwenye maeneo ya Mashariki na Mpakani mwa DRC na Rwanda.
 
Pendekezo hilo limepingwa vikali na nchi ya Rwanda, huku baadhi ya Mataifa yakionesha wasiwasi wao iwapo ndege hizo zitaidhinishwa kutumika kuongezea nguvu vikosi vya MONUSCO katika kuimarisha usalama nchini humo.

Iwapo Baraza la Usalama litaidhinisha mpango huo itakuwa ni maraya kwanza kwa UN kupitisha mpango kama huo nchini DRC mpango utakaosaidia pia kukabiliana na Waasi.(CHANZO:RFI)

UJERUMANI YATUMA WANAJESHI NA MAKOMBORA UTURUKI








Wanajeshi wa Ujerumani wakiiandaa mitambo ya kuzuia makombora, maarufu kama Patriot.

BERLIN-UJERUMANI,
Jeshi la Ujerumani hapo jana (08.01.2013) limetuma wanajeshi wa kwanza nchini Uturuki, kama sehemu ya makubaliano ya Jumuiya ya Kujimhami NATO, kuilinda nchi hiyo dhidi ya makombora kutoka Syria.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere. 
Wanajeshi hao karibu 40 wameungana na wenzao kutoka Uholanzi, nchi nyingine inayomiliki mitambo ya Patriot, inayotumika kuzuia makombora. Mitambo ya Patriot ya Ujerumani pia inasafirishwa leo kuelekea nchini Uturuki.
  
  
Serikali ya Ujerumani imekuwa ikisisitiza mara kwa mara: kwamba kupelekwa kwa wanajeshi wake katika mpaka wa Uturuki na Syria si kwa nia ya kushiriki mapambano. Imesema wanajeshi hao hawatajihusisha na mgogoro unaoendelea nchini Syria, na hili ndio jambo ambalo waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere amelipa umuhimu katika ufafanuzi wa mpango huu. "Harakati hizi ni makhsusi kwa ulinzi na hatua za tahadhari katika eneo la NATO, na hapa kwa ajili ya kulinda mipaka ya Uturuki," amesema waziri De Maziere.
Uturuki  ikiwa ni mwanachama wa NATO  iliwaomba washirika wake kuisadia na sasa ombi hilo limejibiwa. Wanajeshi wa kwanza  wa Ujerumani wanawasili nchini humo na watafanya kazi na wanajeshi wa Uholanzi kuandaa eneo itakapowekwa mitambo hiyo ya Patriot. Mitambo ya Ujerumani inasafirishwa leo kwa njia ya bahari kutoka bandari ya Travemünde kuelekea nchini Uturuki. Awamu nyingine ya wanajeshi wa Ujerumani yenye jumla ya wanajeshi 350 watapelekwa nchini Uturki wiki ijayo.
Dhamira hii ni ishara muhimu ya mshikamano na Uturuki, amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle na kuongeza kuwa: "Tusisahau kuwa kuna mauaji yamefanyika nchinin Uturuki kutokana na mashambulizi kutoka Syria. Hili ndiyo hasa linaloipa wasi wasi Uturuki, kwa sababu hakuna anayejua utawala wa Syria bado unaweza kufanya nini."Katika  kuilinda Uturuki, mitambo hiyo ya Patriot inaweza kuzuia mashambulizi ya roketi, makombora ya masafa marefu na hata kuyadungua baadhi yake. Lakini mitambo hiyo haiwezi kuzuia kitisho kikubwa kama vile mashambulizi ya mizinga. Kwa hivyo hatua hii inapaswa kueleweka kuwa ni ya kiishara zaidi, na kazi yake hasa ni kuzuia, amesema waziri wa ulinzi Thomas de Maziere.
Uwezo wa mitambo ya Patriot
Ujerumani itaiweka mitambo yake katika eneo la Kahramanmaras, karibu kilomita 100 kutoka mpaka wa Syria. Hii ndiyo operesheni ya kwanza ya kweli kwa mitambo ya patriot kutumika baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Bunge la Ujerumani lilipiga kura kwa wingi katikati ya mwezi Disemba kuruhusu kupelekwa kwa mitambo hiyo, na imeruhusiwa kukaa huko hadi mwezi Februari mwaka 2014.Gharama za operesheni hiyo kwa serikali ya Ujerumani zinakadiriwa kuwa euro milioni 25. (CHANZO:DW)




MEMBE NA BASHE NGOMA NZITO CCM


DAR ES SALAAM -TANZANIA,
MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.
Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.

Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.

“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.

Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania.

“Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi.
Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.

Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo.
“Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.
Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”

Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.

Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”

Mgororo ulikoanzia
Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.(CHANZO:MWANANCHI).