Saturday, July 27, 2013

Polisi kwa kumwambukiza mtoto VVU


 
“Sasa nikawa najiona ninaanza kutokwa na vipele sehemu ya mbele na nyuma vinawasha sana na nimejikuna na sasa vimekuwa vidonda na vinatoa  harufu kali.’ Mtoto  wa miaka 15 

Dar es Salaam. Mkazi wa Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpa mimba na kumwambukiza,Ukimwi mtoto wa umri wa miaka 15.
Pamoja na kumwambukiza magonjwa, mtuhumiwa pia anadaiwa kuharibu sehemu za siri na nyuma ya maumbile ya mtoto huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Amana.
Mtuhumiwa wa tukio hilo ni  mlinzi wa minara ya simu, na inadaiwa kuwa alimshawishi mtoto huyo aliyekuwa anafanya kazi za ndani, aache kwa madai kuwa anamtafutia kazi yenye kipato kikubwa.
Akisimulia mkasa huo, katika Hospitali ya Amana alikolazwa, huku akitoa machozi, mtoto huyo alisema “mimi natokea Masasi mkoani Mtwara. Mama mmoja wa Mbagala alikuja kunichukua kwa ajili ya kumfanyia kazi za ndani lakini alinifukuza kazi akisema sijui kazi,”alisema na kuongeza:
“Nilihangaika na nikapata kazi za ndani kwa mama mmoja wa Gongo la Mboto ambako baba huyu mlinzi wa minara ya simu aliniambia niache kazi, niliyokuwa ninalipwa Sh20,000 na niende kufanya kazi yenye malipo ya Sh40,0000”.
 Alidai kuwa baada ya kutoroka kwa aliyekuwa akimfanyia kazi awali, alihamia kwa mlinzi huyo aliyekuwa amepanga eneo la  Vikongoro, Chanika iliyopo Manispaa ya Ilala na kukaa huko kwa madai atampeleka kwenye kazi hiyo.
Alidai uhusiano wao alipokuwa akienda sokoni na hata baada ya kuhamia kwake alilazimisha kumingilia kimwili na kinyume na maumbile. “Ikawa anafanya hivyo...kila siku akitoka kazini alikuwa ananilazimisha kufanya tendo la ndoa hivyo alikuwa ananiingilia mbele na nyuma na kunisababishia maumivu.  Nikimwambia naumia ananitishia sin’topata hata hiyo kazi yenyewe” na kuongeza:
“Sasa nikawa najiona niko tofauti,nikaanza kutokwa na vipele sehemu ya mbele na nyuma vinawasha sana na nimejikuna na sasa vimekuwa vidonda hivi hapa (anamwonyesha mwandishi) hata mwenyewe unaona na vinatoa  harufu kali”.
Akaongeza kuwa baada ya kuona  vidonda vimezidi, kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa anachemsha maji ya moto huku yakichanganywa na dawa kwa ajili ya kujikanda sehemu zilizoathirika.
Amesema licha ya kuathirika hivyo, mwanaume huyo alikuwa akimzuia kutoka nje ya nyumba hiyo na alikuwa akioga na kujisaidia kwenye chumba hicho hadi anaporudi kazini mwanaume huyo na kumwaga huku chakula akiletewa na wakati mwingine analala bila kula.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala , Marietha Minangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema, upelelezi haujakamilika na mtuhumiwa yupo kituo kidogo cha Polisi Stakishari kwa mahojiano zaidi. Ili kupata taarifa zaidi juu ya mkasa huu usikose kusoma Mwananchi Jumamosi.

KATIBA : Dk Mvungi alazimika kuhubiri dini Misenyi


 

 
Na Editha Majura, Mwananchi 
Wajumbe 96 wa Mabaraza ya Katiba, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, wamekutana kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, kwa lengo la kuiboresha, kazi itakayodumu kwa siku tatu.
Akifungua mkutano huo jana, Afisa Utumishi wa wilaya hiyo, Donard Nssoko, alitaka wajumbe hao watoe maoni kwa niaba ya wananchi  ili Katiba ijayo iwe yenye maslahi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika hali inayoashiria kuwa, tume imedhamiria kudhibiti wajumbe wa mabaraza hayo,wasiingize maoni yanayotokana na shinikizo la makundi ya kisiasa, kidini na kiuana harakati, mbinu mbalimbali za kubadili fikra za wajumbe hao zilitawala ufunguzi wa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Tume mkoani humo, Dk, Sengondo Mvungi aligeuka muhubiri alipokuwa akielekeza namna wajumbe wanavyotakiwa kutekeleza jukumu hilo, baada ya maelezo yake kulenga kujenga hofu ya Mungu ndani ya wajumbe.
“Mmetumwa na wananchi siyo mjigeuze tume, bali mboreshe maoni yao kwa kuandika kila kitakacholetwa na mjumbe, ili kikafanyiwe kazi na tume; kushiriki kwenu kuunda sheria kuu kwa Watanzania siyo suala la kibinadamu, bali Mungu amekushirikisha ufanye kazi hiyo kwa niaba yake,” alieleza Dk, Mvungi
Dk. Mvungi aliwataka watambue kuwa hawapo kutumiwa na makundi fulani, kuchakachua kwa kubadili maoni ya wananchi yaliyo katika rasimu, bali kuyaboresha na kwamba kama ilivyo kwa imani za Kikristo na Kiislamu, kwamba wanaoshiriki kujenga Kanisa au Msikiti wamebarikiwa.
Alisema kidunia, wanaoshiriki kuunda Katiba ambayo ni sheria kuu ya nchi, wamebarikiwa na kwamba kinyume na baraka za Mungu ni laana, hivyo akaasa wanapotekeleza jukumu hilo, wajitambue kuwa wanamtumikia Mungu kwa ajili ya watu wake wa Tanzania.
“Mimi siyo Padri, Askofu wala Sheikh nakuelekeza haya, ili ufahamu kuwa usipokuwa mwaminifu kwa Mungu na taifa lako katika hili, hutapata nafasi ya kujitetea mbele za Mungu, msije mkasema hatukujua kuwa kazi ya kutunga Katiba ni ya Mungu; ukikosea utahukumiwa,” Dk. Mvungi alieleza
Mjumbe wa Sekretalieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Marlin Komba kabla ya kufungua mkutano huo, alitoa karatasi kwa kila mjumbe ili iandike wadhifa na sifa yake katika jamii aliyotoka. Vikakusanywa na kuhifadhiwa kwenye bahasha moja.
“Vyeo na sifa zenu zimehifadhi kwenye bahasha hii, ukumbini mmebaki wajumbe wa mabaraza ya Katiba, mtakaoboresha rasimu ya Katiba ili ipatikane Katiba itakayokidhi mahitaji ya Watanzania siyo kwa maslahi ya dini, siasa au uanaharakati,” Komba alieleza
Kama hiyo haitoshi, mwisho wa maelekezo ya tume, Komba aliongoza mabaraza hayo kuimba ubeti mmoja wa wimbo wa taifa, akihimiza kuzingatia umuhimu wa kumshirikisha Mungu na kuzingatia utaifa katika kazi wanayotakiwa kufanya.
Baadhi ya wananchi walionekana kupendelea zaidi makundi fulani ya wananchi, mambo ambayo yanaonekana wazi kwamba yanaweza kuifanya katiba isizae matarajio ambayo wengi wanayo ya kuwepo kwa katiba iliyo safi kwa wote.

Mishahara mipya serikalini 2013


 
Madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakimuudumia mgonjwa hospitalini hapo. Wafanyakazi wa sekta ya afya ni miongoni wa walio ongezewa mishahara na serikari katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14. Picha na Maktaba 
Dar. Serikali imetangaza mishahara mipya kwa watumishi wa umma itakayoanza kutumika mwezi huu, huku kima cha chini kikiongezwa kwa asilimia 41.18 kutoka Sh 170,000 hadi Sh240,000.
Vilevile, mishahara ya watumishi wengine wa umma imeongezwa kwa wastani wa asilimia 8.41. Waraka namba moja kwa watumishi wa umma uliotolewa na Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi Julai 2 mwaka huu, unaeleza kuwa marekebisho hayo ya mishahara yatahusu watumishi wa serikali kuu na watumishi wa serikali za mitaa.
Wengine watakaonufaika na marekebisho hayo ni watumishi walioshikizwa kwenye taasisi za umma na watumishi ambao watakuwa kwenye likizo inayoambatana na kuacha kazi, kustaafu kazi au kumaliza mikataba baada ya Julai mosi mwaka huu.
Waraka huo umeonyesha kuwa watumishi wa serikali ambao wanapata mishahara binafsi isiyo ndani ya viwango vya mishahara ya serikali hawatahusika na marekebisho hayo.
Mei 29 mwaka huu, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, aliliambia Bunge, kwamba Serikali imekamilisha majadiliano ya kuongeza kima cha chini cha mshahara katika sekta 12 binafsi, kitakachoanza kutumika rasmi Julai mosi.
Waziri Kabaka alitaja sekta hizo kuwa ni ya Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati, Viwanda na Biashara, Hoteli na Huduma za Majumbani, Ulinzi Binafsi, Madini, Afya, Uvuvi na Huduma za Majini, Usafirishaji, Mawasiliano na Kilimo. Kwa mujibu wa Kabaka, mishahara imepanda kwa kiwango cha asilimia kati ya 21 na 65 huku Afya ikiongoza kwa kuongezwa ikifuatiwa na sekta ya hoteli na huduma za nyumbani yenye asilimia 55.
Mei mosi mwaka huu akiwa mkoani Mbeya, Rais Jakaya Kikwete, aliahidi unafuu wa maisha kwa wafanyakazi kwa kuangalia uwezekano pia wa kupunguza kodi kwenye mishahara, Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE).
Kuhusu kuongeza mishahara, Rais Kikwete aliahidi wafanyakazi wote kwamba Serikali itaendelea kuiongeza kulingana na hali ya uchumi wa nchi. Waraka huo unaonyesha kuwa mishahara mipya kwa watumishi wa serikali kada ya masharti (operational service), ngazi ya mshahara na mshahara mpya kwenye mabano ni;
TGOS A
TGOS A 1. (Sh240,000), TGOS A 2. (Sh245,600), TGOS A 3. (Sh251,200), TGOS A 4. (Sh256,800), TGOS A 5. (Sh262,400), TGOS A 6. (Sh268,000), TGOS A 7.(Sh272,000), TGOS A 8(Sh279,000), TGOS A 9.(Sh284,800), TGOS A 10(Sh290,400), TGOS A 11(Sh296,000), TGOS A 12(Sh301,600), TGOS A 13(Sh 307,200), TGOS A 14(Sh312,800), TGOS A 15(Sh 318,400), TGOS A 16(Sh324,000), TGOS A 17(Sh329,600) na TGOS A 18(Sh335,200).
TGOS B
TGOS B 1. (Sh347,000), TGOS B 2. (Sh356,500) TGOS B 3 . (Sh366,000), TGOS B 4 . (Sh375,500), TGOS B 5. (Sh385,000), TGOS B 6. (Sh394,500), TGOS B 7. (Sh404,000), TGOS B 8. (Sh413,500), TGOS B 9. (Sh423,000), TGOS B 10. (Sh432,500), TGOS B 11 . (Sh442,000) na TGOS B 12. (Sh451,500).