Saturday, December 08, 2012

MPINZANI WA MNYIKA AKUBALI YAISHE.


DAR ES SALAAM-TANZANIA, ALIYEKUWA mgombea Ubunge katika Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, kupitia CCM, Hawa Ng’humbi amebwaga manyanga na kuachana na rufaa ya kupinga ushindi wa John Mnyika (Chadema).

Rufaa hiyo ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha ubunge wa Mnyika, ilikuwa ianze kusikilizwa jana na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Nathalia Kimaro, Salum Massati na Catherine Oriyo.

Mahakama ya Rufani ilikubali kuondolewa mahakamani hapo kwa rufaa hiyo bila gharama, baada ya mkata rufaa kufikia makubaliano na Mnyika nje ya Mahakama.

Uamuzi wa kuiondoa mahakamani rufaa hiyo ulitolewa jana na kiongozi wa jopo la majaji, Jaji Kimaro muda mfupi kabla ya kuanza kusikilizwa kwake. Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kameya alisema walikuwa tayari kwa usikilizwaji.

Hata hivyo, wakili wa Ng’humbi Issa Maige aliieleza Mahakama kuwa mrufani (Ng’humbi) na Mrufaniwa wa pili (Mnyika), wamekubaliana nje ya Mahakama kuiondoa kesi hiyo bila gharama. “Ni kweli rufaa hii ilikuja kwa ajili ya kusilizwa leo, lakini siku mbili zilizopita, mrufani na mjibu rufaa wa pili, walikutana na kuzungumza na kukukubaliana kuiondoa mahakamani bila gharama,” alisema Wakili Maige na kuongeza: “Hivyo chini ya Kifungu cha 102 (3) na (4) cha Kanuni za Mahakama ya Rufani, ninaiomba Mahakama iiondoe rufaa hii, bila gharama.” Mahakama hiyo ilikubali maombi hayo.

Kwa uamuzi huo, Mnyika ataendelea kuwa Mbunge wa Ubungo hadi atakapomaliza kipindi chake mwaka 2015.

Uamuzi huo ulipokewa kwa shangwe na wafuasi cha Mnyika na Chadema kwa jumla, ambao alizungumza nao kuhusu mikakati yake baada ya kesi hiyo kumalizika. Baada ya mazungumzo hayo Mnyika na wafuasi hao waliamua kuondoka mahakamani hapo kwa kutembea kuelekea ofisi za chama hicho, Kinondoni.

Nje ya Mahakama
Akizungumzia uamuzi uliofikiwa baina ya mteja wake, Ng’humbi, Wakili Maige alisema ni hatua nzuri kwa kuwa inakwenda sambamba na sera ya nchi ya kutaka kupunguza mashauri mahakamani. Alisema baada ya Ng’humbi kutafakari na kuangalia muda uliobakia kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, aliamua kukubalina na Mnyika nje ya Mahakama ili kuiondoa mahakamani rufani hiyo, huku akisema kuwa hatua hiyo pia inaondoa usumbufu na kuokoa muda wa Mahakama.

Mnyika kwa upande wake, alisema siku chache zilizopita Wakili huyo wa Ng’humbi alimpigia simu wakili wake, Edson Mbogoro akimweleza kuwa mteja wake angependa wakutane wazungumze ili waiondoe mahakamani rufani hiyo na kwamba kusiwe na malipo ya gharama za kesi.

Alisema uamuzi huo umethibitisha kuwa ushindi wake ulikuwa ni halali na kwamba sasa atafanya kazi bila wasiwasi.
“Nilipopata taarifa hizo tukashauriana nikaona ni jambo jema kusamehe. Hivyo tumesamehe gharama zote za kesi katika ngazi ya rufaa,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, alisema msamaha huo hauhusu gharama za kesi ya Mahakama Kuu kwa kuwa ilishauriwa lakini akasema hata hilo linazungumzika ikiwa Ng’humbi ataomba hivyo.
Mnyika hakubainisha ni gharama kiasi gani alikuwa ametumia katika kesi hiyo akisema ni mpaka pale watakapofanya mchanganuo.

Kwa upande wake, Wakili Mbogoro alisema mbali na gharama nyingine katika kesi ya msingi, tayari kuna Sh9 milioni walizoziweka mahakamani kama dhamana ya kesi.(CHANZO:MWANANCHI)

MAGUFULI AMPIGIA DEBE RAILA ODINGA.


NAIROBI-KENYA,WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsavangirai kumpigia debe mgombea wa urais wa Kenya, Raila Odinga huku akisema mgombea huyo kupitia Chama cha Orange Democratic Party (ODM), anastahili kuwa Rais wa nchi hiyo kutokana na sifa zake za uongozi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ODM jana, Dk Magufuli alisema hakuna sababu zozote zitakazowafanya Wakenya wasimchague Odinga.
“Nataka kuwaambia Wakenya kwamba Odinga ni mcha Mungu, mnatakiwa kujua hilo. Kama mimi ningekuwa Mkenya ningempigia huyu jamaa kura ili aongoze nchi. Lakini sasa kwa kuwa siruhusiwi hata kupiga kura, basi nawaambia msiache kumchagua huyu atawaongozeni vizuri,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema kati ya wagombea wote waliojitokeza kuwania kiti cha urais nchini Kenya, hakuna anayemfikia Odinga na hiyo inaonyesha kuwa wakimchagua atawasaidia bila ubaguzi.
Alisema na hata Odinga ambaye ni Waziri Mkuu wa Kenya akiamua kugombea ubunge katika Jimbo lake la Chato, hawezi kumshinda.
“Kwa hiyo nasimama hapa ndugu zangu wana ODM kuwapa pongezi kubwa sana, mmmefanya kitu kikubwa sana kwa sababu mmechagua jembe,” alisema.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wajumbe wa mkutano huo, Dk Magufuli alisema kama angekuwa akipiga kura angempa Odinga kura zake zote kwa sababu ni mtu mwenye upendo, uvumilivu, asiye na makuu wala ubaguzi na anayependa kushirikiana na watu wote.
Alisema Odinga ni mpenda amani na kusisitiza kuwa amelisema hilo kwa sababu amani ni muhimu katika maendeleo ya Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.
Alikipongeza chama hicho kwa kuamua kushirikisha vyama zaidi ya 15 na kuweka nguvu zao pamoja ili kushinda katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 4, 2013.
Akizungumzia uhusiano wake na Odinga, Dk Magufuli alisema walifahamiana tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi wa Kenya wakati yeye akiwa Waziri wa Ujenzi wa Tanzania.
“Uliwahi kufika Tanzania mara nyingi na hata kuhudhuria mazishi ya baba yangu mpendwa, ukaja na mawaziri zaidi ya watano pamoja na mke wako katika jimbo langu ninalotoka linaloitwa Chato,” alisema.
Bila kuwataja majina, aliwapiga vijembe baadhi ya wagombea wengine nchini Kenya akisema hawawezi kutembea nje ya nchi hiyo kutokana na kubanwa na sheria, huku akisema Odinga ana uwezo wa kutembea ulimwenguni kote bila pingamizi.
Kuhusu Muungano wa vyama vya kisiasa nchini humo, Dk Magufuli alisema hiyo inaleta changamoto kwa siasa za Kenya… “Huu ni muungano mzuri ambao naukubali sana, hususan walioungana na Odinga ni dhahiri kabisa kwamba wanamtabiria ushindi mkubwa.”
Alisema Wakenya wanatakiwa kuachana na uongozi wa makabila akisema hautawafikisha popote kwani ni kikwazo cha maendeleo na pia ndicho chanzo cha migogoro nchini humo.
“Msilete ukabila… mtakuwa mnaivuruga Kenya yote, watu watakufa, watakosa uhuru wa kuishi sehemu moja kama Waafrika wengine,” alisema.
Alisema vurugu zinazofadhiliwa na utawala uliopo madarakani na ukandamizaji wa washiriki wengine wa shughuli za kisiasa hauhalalishi uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Aliwaonya wajumbe hao kutorudia tena kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo sasa kwa kuwa Serikali ya aina hiyo hujenga chuki kati ya viongozi na kudhoofisha utendaji wa Serikali.(CHANZO:MWANANCHI)

KENYA,TANZANIA,UGANDA WAFUNGUA MIPAKA KWA WATAALAMU

ARUSHA-TANZANIA

Nchi tatu za Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda zimekubaliana kutambua makubaliano kuhusu watalaamu wa kiufundi yatakayowaruhusu watalaamu hao kuingia na kufanya kazi wakiwa huru katika nchi hizo.

Hafla ya kusainiwa kwa makubaliano ilifanyika mjini Arusha Tanzania.
Burundi na Rwanda ambazo pia ni wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki hazikushirikishwa kwenye makubaliano hayo kutokana na ukosefu wa watalaamu wa kiufundi katika nchi zao.

Akizungumzia hatua hiyo, mkurugenzi wa miundo mbinu wa Afrika Mashariki Bw Philiph Wambugu amesema makubaliano hayo ni chombo muhimu cha utekelezaji wa soko huria la pamoja ambalo linafikia mwaka wake wa tatu tangu lianzishwe mwaka wa 2010.(CHANZO:TEHRAN)