Saturday, December 22, 2012

TAIFA STARS VS CHIPOLOPOLO LEO.


DAR ES SALAAM-TANZANIA,
NAHODHA aliyeiwezesha Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo) kuandika historia ya kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu, Christopher Katongo leo anakiongoza kikosi hicho katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katongo, mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka BBC mwaka huu, atakikabili kikosi cha Stars katika mechi hiyo ya kihistoria na pekee kwa aina yake kwa timu hizo mbili.
Hii ni mara kwa kwanza kwa Zambia inayoshika nafasi ya 34 kwa viwango vya ubora katika Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kucheza na Stars inayoshika nafasi ya 130, kama bingwa mtetezi wa mataifa ya Afrika.

Hata hivyo, mara ya mwisho kabla ya mchezo wa leo, zilikutana mwaka jana wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa, shukrani kwa bao la Felix Sunzu lililoipa ushindi wa bao 1-0 Zambia dhidi ya Stars.
Chipolopolo ilitwaa taji la Afrika baada ya kuifunga timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa sehemu mbambali duniani, Ivory Coast.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Chipolopolo Patrice Beaunelle alisema haifahamu vizuri Tanzania kwa miaka ya karibuni, na kwa sababu hiyo anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu na upinzani mkali.
Beaunelle alisema kwa vile, haifahamu vizuri Stars inayofundishwa na Kocha Kim Poulsem, atakipanga kikosi chake kamili wakiwamo baadhi ya chipukizi walioonyesha kiwango kinachovutia.

Mbali na Katongo, wengine watakaoshuka dimbani kuivaa Stars ni
Felix Katongo,Isaac Chansa, Francis Kasonde na Given Singuluma.
Pia anatarajia kuwasili wachezaji wengine waliochelewa kujiunga na wenzao, ambao ni Stophira Sunzu na Rainford Kalaba.

Kwa upande wake Kocha Poulsen atakayeshusha kikosi kitakachowakosa wachezaji wa kulipwa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu amesema mchezo utakuwa mgumu kwa vile wanakutana na timu yenye uwezo mkubwa.
Pia hatakuwa na mshambuliaji wake nyota, John Bocco aliyeumia wakati wa mazoezi, kama ilivyo kwa Samata na Ulimwengu ambao tangu kuwasili wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao kwa sababu ya kuwa majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Poulsen alisema pamoja na kukosekana kwa wachezaji hao bado ana matumaini ya kuisimamisha Zambia inayojiandaa kwenda kutetea taji lao nchini Afrika Kusini mwezi ujao.

"Naipongeza Zambia kwa kukubali kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki, tuna kila sababu ya kujivunia lakini hilo halitatufanya tucheze kwa kuiogopa," alisema Poulsen.
"Natumaini mechi hii itatusaidia kujifunza mengi na pia itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu yetu kwa ajili ya mechi mbalimbali zilizopo mbele yetu za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia pamoja na zile za mashindano ya CHAN.

"Nawaomba Watanzania wajitokeza kwa wingi na kutuunga mkono katika mchezo huu na kukosekana kwa Samata, Ulimwengu na Bocco isiwe sababu ya kutokutuunga mkono," alisema Poulsen.(CHANZO:MWANANCHI)

BARAZA LA USALAMA-UN LAIDHINISHA UVAMIZI WA KIJESHI MALI

NEW YORK-MAREKANI,Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UN kwa pamoja wameidhinisha azimio la kupeleka vikosi vya kigeni kaskazini mwa Mali ili kupambana na Makundi ya kiislamu yenye msimamo Mkali yanayoshikilia eneo hilo tangu mwezi machi mwaka huu

Azimio hilo limepitishwa na Wanachama kumi na tano wa Baraza la usalama la umoja huo na kutoa muda wa kuchukua hatua za lazima kusaidia Serikali ya Mali kurudisha maeneo yanayokaliwa na Wapiganaji wa Kiislamu.

Hata hivyo pamoja na kupitishwa kwa Azimio hilo, Baraza limetaka kufanyika mazungumzo kati ya serikali na makundi ya wapiganaji ili kupata suluhu ya kisiasa nchini Mali.

Mataifa ya Afrika magharibi yamesema tayari yana vikosi 3300 vilivyo tayari kuingia Mali, kulijengea uwezo jeshi la Mali na kusaidia Operesheni za kijeshi nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya UN, takribani watu 400,000 wamepotea tangu kuzuka kwa machafuko hayo mwezi machi mwaka huu.

DK.MWAKYEMBE ATIMUA WENGINE 16 BANDARI.


Dk Mwakyembe atimua wengine 16 Bandari

DAR ES SALAAM-TANZANIA 
Baada ya kuwasimamisha viongozi saba, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Ephraim Mgawe, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameendelea na juhudi za kutaka kuirejeshea hadhi mamlaka hivyo, na safari hii amewasimamisha kazi viongozi wengine 16.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana alipozungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, akisema uamuzi wake umekuja baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo mengi yanayokwamisha ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Alisema Bodi mpya ya TPA ilikutana na kupitia taarifa ya uchunguzi na baada ya kuipitia walichoamua ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wengine 16 na kufanya jumla ya viongozi waliosimamishwa na kuandikiwa barua za kujieleza hadi sasa kufika 23.
Mwakyembe alisema hatua ya kuwasimamisha wengine itaendelea itakapobainika nao wamefanya makosa.
Alisisitiza kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha hadhi ya bandari inarejeshwa na kuboreshwa zaidi baada ya kubainika kuwepo kwa mapungufu mengi yaliyosababisha kupungua kwa ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uhandisi, Mhandisi Mwandisi Bakari Kilo, Meneja Uhandisi, Mhandisi Raymond Swai, Ofisa Mhandisi Mkuu, Mary Mhayaya, Mkurugenzi wa Mipango, Florence Nkya, Meneja Ugavi na Ununuzi, Bahebe Machibya na Meneja Kitengo cha Ununuzi (PMU), Theophil Kimaro.
Wengine ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Ayoub Kamti, Meneja Makasha, Mathew Anthony, Mkurugenzi wa Mifumo ya Menejimenti,
Dk Maimuna Mrisha, Meneja TEHAMA, Marcelina Mhando, Ofisa Ulinzi, Fortunatus Sandaria, Kitengo cha Marine Fadhili Ngorongo, KOJ Opereta Owen Rwebangira, Diver Mohamed Abdullah na Opereta Kilimba.
Aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyobainika kwa mujibu wa taarifa hiyo ya uchunguzi kuwa ni kuwepo mgongano wa kimaslahi ambapo viongozi wa ndani ya mamlaka hiyo wamekuwa na kampuni zao ndogo ndogo zinazohudumia bandari.
“Huwezi kuendeleza mamlaka ya bandari kwa mtindo huu. Kama una maslahi yako huwezi kusimamia shughuli za mamlaka ipasavyo. Kama hiyo haitoshi tumekwenda hadi Brela hizo kampuni hazijasajiliwa, ni za mfukoni tu,” alisema.
Alisema wote waliobainika kuwa na kampuni hizo wameandikiwa barua wajieleze, kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria. Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe ametoa onyo kwa wale wote walioingia katika ajira kwa mipango bila sifa wajiondoe wenyewe kabla hawajafukuzwa kazi.
Alisema moja ya kikwazo cha ufanisi katika mamlaka hiyo ni ajira kutolewa bila kufuata taratibu na Sheria za Nchi na kuonya kuwa wale wanaojijua wameajiriwa kwa mtindo huo waache kazi wenyewe ili walipwe mafao yao badala ya kusubiri kuachishwa na kupoteza kila kitu.
Waziri Mwakyembe pia alizungumzia tatizo la kukithiri vitendo vya wizi ambavyo alivielezea kuwa na mtandao mkubwa. Hata hivyo, alisema tatizo hilo litakomeshwa kabisa.
“Haiwezekani kuruhusu hali hii iendelee. Inakuwaje kontena nzima inayeyuka kama kiberiti, huu ni mtandao mkubwa lazima tuukomeshe kabisa,“ alisema.
Alisema inatia aibu kuona mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi ni Sh milioni 27 hadi 28 kwa mwezi wakati Mombasa ni Sh bilioni tatu. Hata hivyo alisema tangu mwezi Septemba ufanisi mzuri umekuwepo hadi mapato yameongezeka.
“Wale walizoea mchezo huu wa kuchuma kwa njia ya wizi nitawakamata, pamoja na wale wanaoiba vitu humu ndani na kufanya biashara ya kuuza kwa kushirikiana na wale deiwaka wanaosimama hovyo kwenye kijiwe nje, nitawakamata pia,” alisema.
Alipiga marufuku utaratibu wa kulipisha mawakala Sh 200 kama pasi ya bandari (port pass) na badala yake ametaka mamlaka
kuweka utaratibu wa kudhibiti watu kuingia hovyo na kuhakikisha kila mmoja ana kitambulisho kinachoeleweka na anajulikana
anakwenda wapi na anakwenda kufanya kitu gani.(CHANZO:HABARI LEO)