Wednesday, July 10, 2013

MAJINA YA WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA TANO HAYA HAPA.



MAJINA YA WAVULANA-CLICK HAPA

MAJINA YA WASICHANA-CLICK HAPA

WATUHUMIWA WA BOKO HARAM WAFUNGWA MAISHA

Wanachama wanne wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Kiislamu la Boko Haram, wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mashambulio ya bomu yaliyosababisha vifo vya watu kumi na tisa.

Wanne hao walipatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza mashambulio ya mabomu katika ofisi za tume ya uchaguzi na kanisa moja mwaka uliopita.

Hukumu hiyo ndiyo kali zaidi kuwahi kutolelwa kwa mwanachama au mshukiwa yeyote wa kundi hilo la Boko Haram.

Kundi hilo limehusika na mashambulio kadhaa ambayo yamesababisha maafa mengi katika maeneo ya Kaskkazini na Kati nchini Nigeria.

Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limekuwa likiwalenga raia wa kawaida na zaidi ya watu elfu mbili wameuawa tangu kundi hilo la Boko Haram kuanzisha uasi mwaka wa 2009, katika juhudi zake za kutaka kuundwa kwa taifa jipya la Kiislamu katika eneo lililo na idadi kubwa ya Waislamu Kaskazini mwa Nigeria.

Hali ya ulinzi Kaskazini mwa Nigeria;

Hali ya hatari, ilitangazwa tarehe kumi na nne mwezi Mei mwaka huu, katika majimbo ya Kaskazini Mashariki ya Adamawa, Borno na Yobe, hatua iliyoishurutisha serikali ya nchi hiyo kutuma zaidi ya wanajeshi elfu mbili kushika doria katika eneo hilo na pia kuvunja kambi za wanamgambo hao.

BANTEKE AOMBA KUONDOKA ASTON VILLA.



Mchezaji wa klabu ya Aston Villa Christian Banteke amewasilisha ombi la kuondoka katika klabu yake na kuachia Chelsea na Aston Villa kuwania kumsajili kwa kitita cha Pauni Milioni 30.

Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka nchini Ubelgiji mwenye umri wa miaka 22 alijiunga na Aston Villa msimu uliopita akitokea klabu ya Genk ya Ubelgiji kwa kitita cha Pauni Milioni 7.

Benteke amekuwa akidaiwa kujiunga na klabu ya Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotsupurs vilabu ambavyo vinatarajiwa kuendeleza mazungumzo na mchezaji huyo.

Uongozi wa Aston Villa unasema kuwa Banteke atasalia kuwa mchezaji wao ikiwa hatasajiliwa hivi karibuni kwa sababu alikuwa amesaini mkataba wa miaka mitatu na timu yake.

Kocha wa Villa Paul Lambert amesema kuwa ameshangazwa na kuhuzunishwa mno na Banteke kuhusu uamuzi wake kwa kile alichokisema mchezaji huyo hakuelewa kuwa mkufunzi huyo alikuwa anaijenga timu hiyo.

Katika hatua nyingine, mawakala wa mchezaji wa kimataifa wa Uruguay Luis Suarez anasema kuwa mchezaji huyo bado ana nia ya kuichezea klabu ya matufa bingwa barani Ulaya.

Klabu ya Liverpool imekataa Pauni Milioni 30 kutoka kwa klabu ya Arsenal ambayo imeonekana kutofutihwa na msimu wake nchini Uingereza.

Suarez alijiunga na Liverpool mwaka 2011 kwa kitita cha Puani Milioni 22 nukta 7 na ameichezea klabu hiyo mechi 96 na kuifungia mabao 51.

MATOKEO YA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO KUTOLEWA LEO

DAR ES SALAAM, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema majina  ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu,  yatatangazwa leo.

Msemaji wa wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema jana kuwa, majina hayo yatatangazwa leo shughuli itakayofanyika katika ofisi za wizara hiyo.

 “Kesho (leo) saa nne, selected (waliochaguliwa) watatangazwa,” alisema Ntambi.

Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema majina ya wanafunzi hao yatatangazwa siku yoyote ndani ya juma hili.

Mulugo jana alisema majina hayo hayajachelewa kutangazwa na kwamba wanafunzi wa kidato cha sita hufungua wiki ya tatu ya Julai na kwamba hata sasa bado hawajafungua.

“Matokeo tutayatoa wiki hii na  hatujachelewa kuyatangaza kwa sababu  kwa kawaida kidato cha tano na sita wanafungua shule wiki ya tatu Julai , kwa hiyo tukitoa wiki hii tutakuwa hatujachelewa,” alisema Mulugo.

Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani jijini Dar es Salaam, alisema kuwa kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti.

“Mpaka sasa hatujaambiwa kwa nini hii hali imekuwa hivi, kwa kawaida kidato cha tano huripoti shuleni wiki moja kabla ya kidato cha sita, lakini mpaka sasa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano bado hawajatangazwa,” alisema Mwalimu huyo.

Wakati majina hayo yakitarajiwa kutangazwa leo, ni dhahiri kuwa shule za Serikali zenye kidato cha tano na sita zitaendelea kupata idadi ndogo ya wanafunzi tofauti na uwezo huku baadhi zisizo za Serikali zikitishia kuachana na biashara ya shule.

Hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa mtihani wa kidato cha nne, ambapo kwa mwaka 2012 waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 35,349. Wwanafunzi walio katika nafasi kubwa ya kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni wale waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.(MWANANCHI)


BIBI HARUSI MTARAJIWA AFARIKI SAA MOJA KABLA YA HARUSI YAKE.

HANDENI,TANGA,Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Bibi Harusi ambaye ni mkazi wa Chanika mjini Handeni, Levina Mmasi (23) amefariki dunia saa moja kabla ya ndoa yake kufungwa katika Kanisa la Katoliki la Roma Wilaya Handeni Jumamosi na hivyo kuilazimu kamati ya maandalizi ya harusi kujigeuza na kuwa ya msiba.

Kifo hicho kilichotokea Jumamosi mwishoni mwa wiki iliyopita, kimekuwa gumzo mjini Handeni huku wananchi wakisema kuwa ni tukio ambalo halijawahi kutokea katika wilaya hiyo.

Msemaji wa familia ya marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Firmin Mrimasha, alisema kuwa chanzo cha kifo cha Levina ambaye alijifungua mwanzoni mwa wiki iliyopita,ilikuwa ni homa aliyoipata ghafla siku ya Alhamisi na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na kukutwa na malaria na kisha kulazwa kwa matibu.

 “Huyu bibi harusi alikuwa ametoka kujifungua, alikuwa na mtoto wa kiume kutokana na ujauzito wa miezi saba, ndipo ghafla Alhamisi akapata homa tukampeleka hospitali alikolazwa na baada ya kupata nafuu, aliruhusiwa Ijumaa.

“Baada ya kuruhusiwa akaanza maandalizi ya harusi na Jumamosi ambayo ndiyo siku ya ndoa yake, alijiandaa lakini ilipofika saa 8.05 akafariki dunia akiwa nyumbani akisubiriwa kwenda kanisani kufunga ndoa ambayo ilikuwa ifungwe saa 9.00,” alisema Mrimasha.

Alisema, “Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani marehemu amefariki saa moja kabla ya ndoa yake na baada ya kifo hicho, mtoto wake naye alifariki muda mfupi baada ya mama yake kufariki dunia,” alisema Mrimasha.

Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harusi hiyo iliyogharimu Sh7.7 milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake ni tukio la kwanza kutokea tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi kulisahau.

“Nilishazipangia kazi kamati za maandalizi, lakini ghafla tukapewa taarifa kuwa bibi harusi amefariki...Hatukuamini, ikabidi niwatangazie wanakamati wenzangu kuwa hakuna tena shughuli, bibi harusi amefariki,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati na kuongeza:

“Kitu tulichokuwa tukisubiri ni kuambiwa bibi harusi angefika saa ngapi, lakini ghafla tukapewa taarifa za kifo, ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli imetokea na inasikitisha kwani si jambo la kawaida,” alisema Kipacha.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni kuwa marehemu alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na kwamba alikuwa katika kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti yanamkuta alikuwa hajapokea hata mshahara wake wa awali.

Akizungumzia hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe ndoa hiyo, Max Sabuni wa kanisa hilo Katoliki Handeni alisema:       “Nimesikitishwa na tukio hili kwa kuwa halikuwahi kunitokea...Kilichobaki ni wanandugu kuwa watulivu kwa kuwa Mungu amechukua kiumbe wake kwa muda alioupanga.”

Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.