Tuesday, February 03, 2015

Huyu amewekewa mikono ya mtu mwingine!


oppp
Madaktari katika Chuo cha Tiba cha Amrita, Kochi huko India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa aina yake wa kupandikiza mikono mipya kwa binadamu aliyekatika viungo hivyo.
Upandikizaji huo uliofanyika Januari 12 na 13, ulifanikiwa kwa mara ya kwanza, baada mwanamume mwenye umri wa miaka 30, aliyekatika mikono katika ajali ya treni kuwekewa mingine ambayo ilichukuliwa kutoka kwa kijana wa miaka 24 aliyefariki katika ajali ya gari.
Mkuu wa kitengo cha upasuaji katika chuo hicho, Prof. Subramania Iyer alisema: “Siku 14 baada ya upasuaji, mikono ilikubaliwa na mwili na ikaanza kujongea, yaani aliyepandikizwa aliweza kuisogeza huku na kule. Mgonjwa alitolewa chumba cha wagonjwa mahututi na huduma nyingine za kumchunguza ziliendelea.”
amrrrr
Moja ya majengo ya chuo cha tiba cha Amrita Kochi
Daktari katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (Moi), Prof. John Kahamba aliliambia Gazeti la MWANANCHI kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa upandikizaji wa mikono kufanyika duniani kwani ina tofauti kubwa na upandikizaji wa figo au ini.
Profesa Kahamba alisema upasuaji huo unafanyika kwa kuhakiki mambo mbalimbali ikiwamo uwiano wa kundi la damu, uhai wa seli na misuli na mishipa midogo ya fahamu.
Profesa Kahamba alisema kama upandikizaji wa figo unavyofanyika, kadhalika upandikizaji wa mikono unahitaji umakini wa muda.
Anasema iwapo utachelewa kuunganisha mikono baada ya kuitoa, seli zake zinaweza kufa na kushindwa kufanya kazi zitakapopandikizwa kwenye mwili.