Monday, March 11, 2013

FIFA YATISHIA KUIFUNGIA TANZANIA



 
Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MTUHUMIWA MKUU WA UBAKAJI INDIA AJINYONGA GEREZANI

Mwili wa Singh ukitolewa gerezani .
Ram Singh 
DELHI-INDIA, Mtuhumiwa  katika kesi ya ubakaji wa msichana mmoja wa chuo kikuu ambaye baadaye alifariki nchini India, amekutwa akiwa  amefariki ndani ya gerezanila Tahir nchini India  alipokuwa akishikiliwa.

Kwa mujibu wa polisi wamesema kuwa Ram Singh, alijinyonga akiwa ndani ya gereza la Tihar mjini Delhi's Tihar, ingawa mawakili wa utetezi wanadai kuwa huenda alinyongwa.
Ram Singh, aliyekua na umri wa miaka 33, alikuwa mmoja wa washukiwa katika kesi ya ubakaji wanaozuiliwa na polisi kwa madai ya mauaji ya msichana waliyembaka.
Wote walikanusha madai hayo.

Shambulizi dhidi ya mwanafunzi huo, lililofanyika Desemba mwaka jana, lilizua mjadala mkali nchini India kuhusu udhalilishwaji na ukatili dhidi ya wanawake.

Washukiwa wengine wa ubakaji bado wanazuiliwa katika gereza hilo.Kesi ya mshukiwa wa sita inaendeshwa katika mahakama ya watoto.

Mwandishi wa BBC Sanjoy Majumder,mjini Delhi,amesema kuwa kifo cha bwana Singh kinakuja kama aibu kubwa kwa maafisa ambao wanakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu kesi hiyo.
Msemaji wa jela hiyo Sunil Gupta, aliambia BBC kuwa Ram Singh alijinyonga kwa banketi usiku wa kuamkia leo.(CHANZO:BBC)

VURUGU ZAANZA KENYA-MWANASHERIA MKUU MSTAAFU KUMTETEA ODINGA


 
   NAIROBI-KENYA,
  Polisi wa kutuliza ghasia juzi walilazimika kutumia mabomu ya machozi Mjini Kisumu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga kutangazwa kwa matokeo ya urais ambayo mgombea wao, Raila Odinga alianguka.
Vurugu hizo ziliibuka, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.
Maelfu ya vijana wamekuwa wakirandaranda kwenye maeneo kadhaa ya Kisumu wakichoma majengo na kufunga barabara, huku wakiimba: “Bila Raila, hakuna amani.”
Vurugu hizo zilizoanza juzi jioni zimesababisha maduka kufungwa huku makundi ya vijana wenye hasira wakiendelea kurandaranda mitaani wakipambana na polisi ambao walifanya jitihada za kuwatuliza na kurejesha amani.
Ilielezwa kwamba, muda mfupi tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi, zaidi ya vijana 100 waliibuka na kuanza kuwarushia mawe polisi na muda mfupi baadaye idadi ya vijana hao iliongezeka na kusambaa katika maeneo karibu yote ya Kisumu.
Odinga ambaye alikuwa mgombea wa Muungano wa Cord, amewataka wafuasi wake kuwa watulivu kwa kuwa anahitaji kufuata mkondo wa sheria kupinga matokeo hayo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa juzi, yalimpa ushindi Kenyatta aliyesimama kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee, wa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 43 alizopata Raila.
Raila atinga mahakamani
Muungano wa Cord, leo utawasilisha vielelezo mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ametajwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la wanasheria watakaopinga ushindi wa Kenyatta.
Jopo hilo la wanasheria linaongozwa na mwanasheria mkongwe, George Oraro na baadhi ya mawaziri wakiwamo; Mutula Kilonzo, James Orengo na Ababu Namwamba ambao ni washauri wakuu wa jopo.
Oraro alimtetea aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Henry Kosgei wakati alipokabiliwa na kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, The Hague.
Wengine wanaounda timu hiyo ni Gitobu Imanyara, Pheroze Nowrojee, Chacha Odera, Ambrose Rachier na Paul Mwangi.
Cord imepanga kufungua kesi ikitaka Mahakama itengue hatua ya kutangazwa kwa Kenyatta kuwa Rais wa Kenya kwa kuwa taratibu za ukusanyaji matokeo zilikiukwa.
Tangu juzi, jopo hilo la wanasheria lilikuwa na vikao mfululizo kuandaa ushahidi wa kesi hiyo ikiwamo kukusanya vielelezo watakavyosimamia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu namba 163 cha Katiba ya Kenya.
Mfuasi wa Uhuru afariki
Shamrashamra za kushangilia ushindi wa Kenyatta ziliingia doa kwenye Mji wa Nyeri baada ya lori lililobeba mashabiki wa mgombea huyo kutumbukia kwenye korongo na kuua mtu mmoja. Katika ajali hiyo watu 30 walijeruhiwa lakini wakiwa katika hali mbaya.
Mwili wa mtu aliyefariki ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Nyeri wakati wengine waliojeruhiwa wamelazwa kwenye hospitali hiyo.(MWANANCHI)