Wednesday, May 22, 2013

RIPOTI YA TUME YAPENDEKEZA KENYATTA NA RUTO KUSHITAKIWA

NAIROBI-KENYA,Viongozi wa ngazi za juu nchini Kenya, wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto, ni miongoni mwa waliopendekezwa kushtakiwa katika ripoti ya kushtusha iliyotolewa na Tume ya TJRC. 


Tume ya maridhiano na haki ilikabidhiwa jukumu la kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa tangu mwaka 1963 nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake.


Iliundwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/08 uliozua ghasia miaka mitano iliyopita kama njia ya kuleta maridhiano miongoni mwa wakenya.

Baada ya uchaguzi huo, watu 1,500 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kulazimika kutoroka makwao.


Kenyatta na Ruto, waliokuwa mahasimu katika uchaguzi wa mwaka 2007, walishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi baada ua kuungana chini ya muungano wa Jubilee.

Licha ya kuwa hakuna mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo dhidi ya Rais na naibu wake, inapendekeza uchunguzi zaidi dhidi ya maafisa wakuu waliotajwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007 na hata kufunguliwa mashtaka.(CHANZO:BBC&DW)

OBAMA KUZURU TANZANIA MWEZI UJAO.



WASHINGTON-MAREKANI,
Ziara ya siku nane ya Rais wa Marekani, Barak Obama na mkewe Michelle katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini na Senegal, imeelezwa kuwa ina lengo la kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa Afrika.

Wakati wa ziara hiyo, itakayodumu kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, mwaka huu Obama atakutana na viongozi mbalimbali wa kiserikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na jumuiya huru za kiraia ikiwamo vijana ili kujadili ubia wa kimkakati katika ushirikano na masuala mengine ya kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu ya Marekani kuhusu ziara ya Rais Obama barani Afrika na Ubalozi wa Marekani nchini kuisambaza katika vyombo vya habari jana, ilisema ziara hiyo itadhihirisha dhamira ya dhati ya Rais huyo kupanua na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi yake na watu wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kuimarisha amani na ustawi katika kanda hiyo na duniani kote.

Ilisema kuwa katika ziara yake hiyo, Rais Obama atawekea mkazo umuhimu ambao Marekani inauweka katika ushirikiano wa kina na unaoendelea kuimarika na nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mipango mbalimbali ikiwamo ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, uwekezaji na biashara, uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia na uwekezaji katika kizazi kipya cha viongozi wa Kiafrika.

 Ziara Rais Obama barani Afrika ni moja ya ahadi zake za kukuza na kupanua ushirikiano kati ya watu wa Marekani na watu wa nchi za kusini mwa Jangwa la SaharaAfrika katika masuala ya kimaendeleo na amani.

Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika. Ziara yake ya kwanza aliifanya wakati wa awamu yake ya kwanza nchini Ghana.

 Rais Obama alianza rasmi awamu yake ya kwanza kama Rais wa Marekani, Januari 20, 2009 na awamu yake ya pili ilianza Januari 21, 2013.

 Ziara ya Rais Obama inafanyika siku chache baada ya ziara ya Rais wa China,  Xi Jiping, ambaye aliyeitembelea Tanzania Machi 28, mwaka huu, na Tanzania ilikuwa nchi yake ya kwanza kuitembelea barani Afrika tangu achaguliwe kuwa rais, Machi 14, mwaka huu.

Baada ya ziara ya Tanzania, Jiping alikwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa mataifa ambayo uchumi wake unakua kwa kasi duniani.

Uchumi wa China unakua kwa kasi kubwa na hivi sasa taifa hilo linatajwa kuwa ni la pili kiuchumi duniani, baada ya Marekani.

China imekuwa ikitajwa kuwa inatafuta ushawishi katika mataifa ya Afrika ili kupata rasilimali kama madini, mafuta, gesi na rasilimali zitokanazo na misitu.

Ziara ya Obama inatazamwa kama njia ya kuendelea kujiimarisha barani Afrika wakati China nayo ikiendeleza kusaka nafasi hiyo pia.(CHANZO:NIPASHE)