Monday, October 22, 2012

Wapiganaji wa kigeni waingia Mali Kaskazini

Mamia ya wanajihadi kutoka nje ya nchi ya Mali wameripotiwa kuwasili kaskazini mwa nchi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita kupigana na wanamgambo wa kiislamu wanaomiliki eneo la kaskazini mwa Mali wakati vikosi vya kimataifa vikitarajiwa kuingilia kati mzozo wa Mali. Wakazi wa Mji wa Timbuktu, Gao na Maafisa usalama wa nchini Mali na Makamanda wa makundi ya kiislam wamethibitisha kuwa kumekuwa na wimbi la wapiganaji wa kigeni wanaoingia kaskazini mwa Mali kwa zaidi ya siku mbili zilizopita. Kuwasili kwa wanajihadi hao kutoka Sudan na Sahara Magharibi, kunatokea siku mbili tu baada ya mkutano wa kimataifa wa nchi washirika wa Mali ambao umedhamiria kuongeza mshikamano na serikali ya Mali kurudisha eneo hilo. Wakati huohuo,Serikali ya Ufaransa inatangaza kurejelea ushirikiano wake wa kijeshi na nchi ya Mali, Ushirikiano ambao ulisimamishwa tangu jaribio la mapinduzi ya tarehe 22 ya mwezi Machi 22 mwaka Wimbi hilo la wapiganaji limeingia wakati huu ambapo jumuia ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika,ECOWAS ikiendelea na harakati za kuvamia kaskazini mwa nchi hiyo na kusambaratisha Makundi ya kiislamu katika eneo hilo.(Chanzo RFI)

MWAKYEMBE AKABIDHIWA RIPOTI YA BANDARI

DAR ES SALAAM-TANZANIA, WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku akitoa onyo kali kwa vigogo waliokwepa kuhojiwa na kamati kwa visingizio mbalimbali akisema ni lazima watahojiwa tu. Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo yenye kurasa 285 na Mwenyekiti, Wakili Benard Mbakileki, na kuongeza kuwa kama suala analotaka kuhojiwa mhusika linahusu polisi, atapelekwa mbele ya jeshi hilo. Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo baada ya Wakili Mbakileki kueleza kuwa baadhi ya watu muhimu TPA waliotakiwa kuhojiwa walikwepa kwa visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima simu kabisa. Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: “Kama walidhani kukwepa kamati ndio mambo yameisha, wanajidanganya. Watakuja kujibu mbele yangu na kama mambo yanahusu polisi tutawapeleka, hatutaacha mtu.” Aliongeza kuwa kamati hiyo imefanya kazi ya kizalendo na kuahidi mambo yote iliyopendekeza watayafanyia kazi hatua kwa hatua, ili kuboresha bandari hiyo. “Niwahakikishie hii kazi mliyoifanya haitakwenda bure, hadi kufikia Desemba mwaka huu, tutakuwa tumeyafanyia kazi mambo yote mliyopendekeza. Tutataka kuipa bandari sura mpya, kwa sasa inakosa ufanisi…tutakuja na uamuzi ambao hakitadokolewa kitu, kwani watakaodokoa, nao watadokolewa, kwani tusipofanya uamuzi huo hatutaikomboa nchi yetu,” alisema. “Tulikuwa tunasikia habari za Twiga kusafirishwa kwenye ndege watu wakashangaa, lakini pale bandarini kontena na ukubwa wake linayeyuka. Mwaka juzi yaliyeyuka makontena 10, mwaka jana 26 na mwaka huu mawili na mambo yanatufanya tusiaminike,” alisema. Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, watafanya kazi kwa gharama yoyote, bila kumwonea mtu, ili kurekebisha bandari hiyo aliyoeleza kuwa iwapo ingesimamiwa vizuri nchi ingeweza kuendesha mambo mengi. Aidha, alibainisha kuwa tangu kamati hiyo ilipoanza kufanya kazi, baadhi ya nchi jirani zimeanza kurejesha imani na bandari hiyo zilikemo Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi. Aliongeza kuwa iwapo baadhi ya watu wanakerwa na mabadiliko ndani ya TPA, waondoke kwani mjini kuna kazi nyingi za kufanya. Pamoja na mambo mengine, Mwakyembe aliomba wapatiwe muda wa kuipitia ripoti hiyo kwa umakini na kwamba kila hatua watakuwa wakitoa taarifa kwa umma.(Chanzo:Bongonewztz)

FIDEL CASTRO AONEKANA TENA



HAVANNA-CUBA,
Kiongozi mwanamapinduzi wa Bw. Fidel Castro(86) ameonekana kuwa katika hali nzuri tofauti na uvumi baada ya kukutana na aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Venezuela Bw. Elias Jaua hapo jumamosi iliyopita.Jaua ambaye ameonesha picha za kiongozi huyo na kuwaambia waandishi wa habari kuwa kiongozi huyo yupo katika hali nzuri.

Fidel Castro hajaonekana hadharani tangu mwezi Machi mwaka huu alipokutana na kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa Benedict XVI.Tangu wakati huo kiongozi huyo hajaonekana hadharani na kuzua utata juu ya afya yake huku wengi wakivumisha yupo mahututi na wengine wakidai amefariki.

Tangu kuonekana kwake mwezi Machi kiongozi huyo amekuwa akitoa hotuba zilizoandikwa kwenye vyombo vya habari bila ya yeye kutokea huku baadhi ya hotuba hizo kuonekana zina dosari kiasi na kuzua maswali kuhusu afya ya kiakili ya kiongozi huyo.

Bw.Jaua ambaye anagombea ugavana katika jimbo la Miranda huko venezuela amesema waliongea na Fidel Castro katika Hoteli ya Havana na waliongea kuhusu mambo mengi yakiwemo kilimo na siasa,"Ndiyo nimeonge na Fidel jana alikuwa vile vile kama yule Fidel wa zamani na mashavu yake ya pink," Martinez aliliambia shirika la Reuters.